Tanzania kuwa ghala la chakula barani Afrika

HomeKitaifa

Tanzania kuwa ghala la chakula barani Afrika

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kutumia vyema fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) kwa kuionyesha dunia nia ya nchi ya kuwa ghala la chakula Barani Afrika.

Rais Samia aliyekuwa akizindua maandalizi ya jukwa hilo leo Machi 17, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam amewaambia wahudhuriaji kuwa ili kutimiza adhma hiyo tayari Serikali imeanza kuwekeza katika maeneo ya kibajeti na kimkakati.

“Tumeanza kuwekeza kibajeti na kimkakati katika maeneo ya msingi ikiwemo kuongeza tija katika uzalishaji kwa kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu bora na wanapata pembejeo kwa wakati, “ amesema Rais Samia.

Samia amesema kuhakikisha vijana wanakuwa kipaumbele katika uwekezaji na  mageuzi ya kilimo nchini kupitia programu ya (Kujenga Kesho bora), kuwekeza katika tafiti na kufungua masoko ya kimataifa pamoja na kujenga miundombinu ya umwagiliaji ni miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa.

AGRF ni mkutano huo wa kila mwaka unawakutanisha watu zaidi ya 3,000 wakiwemo viongozi, watunga sera, wanasayansi, wakuu wa serikali na taasisi za binafsi, wakulima, na vijana ili kujadili na kutafuta suluhu ya usalama wa chakula barani Afrika na maisha bora kwa wote.

Mkutano huo unatajwa utachangia kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya kilimo nchini, kukuza utalii, kuimarika kwa masoko na teknolojia barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Wakati Serikali ikichukua hatua kadhaa kuimarisha changamoto zilizopo kwenye sekta ya kilimo, Rais Samia amemtaka Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega kuongeza ubunifu utakaoleta matokeo yenye tija katika sekta ya mifugo na  uvuvi kwani kilimo ni sekta pana na haihusishi mazao peke yake.

“Tunapozungumza kilimo watu wengi watadhani tunazungumza kilimo cha mazao, kilimo ni pamoja na uvuvi pamoja na ufugaji, Waziri wa Uvuvi mwezi Septemba tunapoonesha maendeleo tuliyonayo tuone kwako mashamba na vizimba vya samaki,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametumia pia fursa hiyo kutangaza Baraza la Kumshauri Rais kuhusu Utekelezaji wa Masuala ya Kilimo ambalo Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda.

error: Content is protected !!