Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel W. Shelukindo amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian leo Septemba 18, 2025 katika ofisi ndogo za wizara, Dar es Salaam na kujadili masuala mbalimbali ya utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano kati ya Tanzania na China.
Viongozi hao wamejadili kuongeza jitihada za ushirikiano katika uwekezaji na biashara pamoja na kuongeza kuungwa mkono katika masuala yanayohusu mataifa hayo mawili katika masuala ya kikanda na kimataifa.
Kwa pamoja wamejadili yatokanayo na mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Juni mwaka huu, ambapo China imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote yaliyoainishwa katika utekelezaji wa maazimio ya mkutano huo.
Viongozi hao wamekubaliana kuongeza nafasi zaidi za mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa wizara katika nyanja ya diplomasia sambamba na watumishi wengine wa Taasisi za Serikali.
Mhe. Balozi Mingjian amemuarifu Balozi Shelukindo kuwa Ubalozi wa China nchini unatarajia kuwa katika likizo ya kusherehekea Siku yao ya Kitaifa, hivyo ofisi zake hazitofanya kazi kwa kipindi kifupi kuanzia Oktoba 1, 2025. Hivyo, Watanzania wenye safari za hivi karibuni hususani mwezi wa Oktoba wanaombwa kufanya taratibu zote mapema, kuepuka usumbufu.