Pembezoni mwa Mkutano wa 47 wa Kawaida wa Mawaziri wa Umoja wa Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Wizara Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mhe. Hadera Admassu ikiwa ni ishara ya dhamira ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano wa uwili baina ya mataifa hayo mawili.
Majadiliano yao yamelenga kuimarisha makubaliano yaliyopo, hasa katika biashara, usalama, na miundombinu.
Viongozi hao wawili wameafikiana kuimarisha ushirikiano wa mataifa yao hasa katika usafiri wa anga, eneo ambalo Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka kwa Ethiopia.
Nchi zote mbili zimethibitisha kujitolea kwao kwa amani ya kikanda, na kuahidi kubadilishana uzoefu katika kusimamia migogoro ya ndani na kukuza utulivu.
Aidha, kwa pamoja viongozi hao wamejadili umuhimu wa kutunza mazingira ikiwemo upandaji wa miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.