Tanzania na Marekani zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.15

HomeKimataifa

Tanzania na Marekani zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.15

Serikali ya Marekani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano Rasmi Katika Sekta ya Afya baina ya nchi hizo mbili ya miaka mitano yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1, zikithibitisha dhamira ya pamoja ya kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, kuboresha afya, na kujenga mfumo wa afya wa Tanzania ulio imara na na uendelevu zaidi. Hafla ya utiaji saini ilishuhudiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Bi. Jeanne Clark, na Waziri wa Afya wa Tanzania, Mohammed Mchengerwa.

Kupitia Mkakati wa Utawala wa Rais Trump wa America First Global Health Strategy (AFGHS) Hati hii ya Makubaliano imewezesha uwekezaji wa pamoja kutoka Serikali ya Tanzania, ambayo imeahidi kuwekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 1.8 katika mifumo yake ya afya katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Serikali ya Marekani, kwa kushirikiana na Bunge la Congress la Marekani nayo inakusudia kutoa zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.3 katika kipindi cha miaka mitano cha utekelezaji wa makubalino haya ili kuendeleza malengo ya pamoja ya afya duniani.

Uwekezaji huu wa pamoja unaonyesha dhamira ya nchi zote mbili ya kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza na kuimarisha uwezo wa Tanzania wa kugharamia, kusimamia na kuendeleza kwa kujitegemea huduma muhimu za afya.

“Hati hii ya Makubaliano inafungua ukurasa mpya wa miaka mitano katika ushirikiano wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika sekta ya afya,” alisema Kaimu Balozi wa Marekani nchini Bi. Jeanne Clark.

“Kwa kuwekeza kwa pamoja, tunaimarisha uwezo wa Tanzania wa kuzuia, kugundua na kukabiliana kwa haraka na vitisho vya afya, huku tukijenga mifumo endelevu na inayoweza kujitegemea ya kutoa huduma bora za afya kwa vizazi vijavyo. Kuimarika kwa kujitegemea na usalama wa afya nchini Tanzania kunawalinda Wamarekani na Watanzania kwa kudhibiti milipuko hatari katika chanzo chake, kabla haijavuka mipaka na kuenea kimataifa.”

Hati hii ya Makubaliano imesainiwa kupitia Mkakati wa Afya Duniani wa “Marekani Kwanza,” unaoweka kipaumbele katika kuokoa maisha na kuwalinda Wamarekani dhidi ya vitisho vya kiafya kabla havijafika katika mipaka ya Marekani, huku ukishirikiana na nchi zinazopokea msaada kuimarisha uwezo wao wa ndani wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza pamoja na dharura nyingine za afya ya umma. Kwa kuimarisha uwezo wa Tanzania wa kushughulikia vitisho vya afya katika chanzo chake, ushirikiano huu utasaidia kulinda afya na usalama wa Watanzania na Wamarekani.

Chini ya Hati hii ya Makubaliano, Marekani na Tanzania zitaimarisha ushirikiano katika kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha miundombinu ya afya kidijitali (digital health infrastructure), kupanua ufuatiliaji wa magonjwa na kuimarisha usalama wa afya. Hati hii pia inaunga mkono jitihada za Tanzania za kuandaa na kutekeleza mfumo mmoja wa kitaifa wa afya kidijitali uliofungamanishwa, ambao umejengwa katika maeneo matano yaliyobainishwa: huduma za kitabibu; ugharimiaji wa huduma za afya na bima ya afya; minyororo ya ugavi; afya ya umma na ufuatiliaji wa magonjwa; pamoja na huduma kwa wananchi.

Waziri wa Afya Mohammed Mchengerwa aliitaja hati hii ya Makubaliano kama hatua muhimu kuelekea kuongeza umiliki wa kitaifa na kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu wa mfumo wa afya wa Tanzania. “Hati hii ya Makubaliano inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania ya kuwekeza katika afya na ustawi wa wananchi wetu,” alisema Waziri Mchengerwa. “Uwekezaji wetu wa pamoja utaimarisha miundombinu ya afya, kuongeza nguvu kazi katika sekta ya afya, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa na kuharakisha maendeleo ya mifumo ya kisasa ya maabara na afya kidijitali. Tunathamini ushirikiano unaoendelea wa Marekani wakati Tanzania ikijenga mfumo wa afya ulio thabiti zaidi, unaostahimili changamoto na unaojitegemea zaidi.”

Vipengele vingine vya Hati hii ya Makubaliano vinajumuisha kuanzishwa na kuanza kazi kwa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Umma ya Tanzania (Tanzania National Public Health Institute) katika ngazi ya kitaifa na ngazi za chini; kuimarisha uwezo wa taasisi za utafiti wa afya nchini Tanzania wa kufanya tafiti za kitabibu; pamoja na kusaidia juhudi za kutokomeza malaria Zanzibar.

Hati hii ya Makubaliano pia inalenga kuanzisha na kuendeleza mtandao wa maabara uliounganishwa, unaoweza kubadilishana taarifa na ulioboreshwa katika ngazi mbalimbali za mfumo wa afya, wenye uwezo wa kufikia viwango vya mfumo wa 7-1-7 wa kugundua na kukabiliana na milipuko. Chini ya mfumo huu, milipuko inayoshukiwa inapaswa kugunduliwa ndani ya siku saba, kuripotiwa kwa mamlaka za afya ya umma ndani ya siku moja, na kukabiliwa kwa hatua madhubuti ndani ya siku saba.

Hati hii ya Makubaliano ya miaka mitano inajengwa juu ya miongo kadhaa ya ushirikiano wa afya duniani kati ya Marekani na Tanzania, na inaashiria hatua muhimu kuelekea kuongeza umiliki wa nchi, ugharimiaji endelevu na ustahimilivu wa muda mrefu wa mfumo wa afya. Kupitia ushirikiano huu, Marekani na Tanzania zitafanya kazi pamoja kulinda jamii zetu dhidi ya tishio la magonjwa ya kuambukiza, kujiandaa kwa vitisho vya afya vya siku zijazo, na kuisaidia Tanzania kufikia kiwango kikubwa zaidi cha kujitegemea na kuhakikisha uendelevu wa mfumo wake wa afya.

error: Content is protected !!