Tanzania na Uingereza kuendeleza ushirikiano sekta za kiuchumi

HomeKitaifa

Tanzania na Uingereza kuendeleza ushirikiano sekta za kiuchumi

Serikali ya Tanzania na Uingereza zimesaini Makubaliano ya Kukuza Ushirikiano (Mutual Prosperity Partnership) yanayolenga kuchochea maendeleo katika sekta za kiuchumi zikijumuisha uwekezaji, biashara na miundombinu.

Makubaliano hayo yameshuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), na Waziri wa Maendeleo wa Uingereza anayeshughulika Maendeleo na Afrika Mhe. Endrew Bower Mitchell (Mb.).

Makubaliano hayo yalitiwa saini na Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa niaba ya Tanzania na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concar kwa upande wa nchi ya Uingereza.

Mhe. Mkumbo ameeleza kuwa malengo makuu ya Makubaliano hayo ni kuwezesha Tanzania kunufaika na fursa za upatikanaji wa mitaji ya utekelezaji wa miradi itakayobuniwa na Serikali pamoja na sekta binafsi kwa sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu itakayofikia paundi za Uingereza bilioni 1 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 3.

Vilevile, makubaliano hayo yanalenga kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi kutoka Uingereza (FDI) wa thamani ya mazingira ya paundi za Uingereza Milioni 300.

Malengo mengine ni kukuza uwekezaji wa sekta binafsi nchini hususan wawekezaji wadogo na wa kati kunufaika na fursa za mitaji ya Uingereza kiasi cha paundi za Uingereza Milioni 100, ambazo ni sawa na zaidi ya Bilioni 300 za kitanzania.

Prof. Mkumbo alisema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Uingereza kwenye sekta ya madini ya kimkakati hasa katika kuongeza thamani ya madini hayo hapa nchini.

“Hii ndiyo nia na lengo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba muda umefika wa kuongeza thamani mazao yetu ya madini hususani madini ya kimkakati yanayohitajika katika kulinda mazingira kwani hutumika kuongeza thamani ikiwemo kutengeneza betri, hatua ambayo itatuongezea faida ya kiuchumi.”

Kwa upande wake Mhe. Andrew Bower Mitchell (Mb.), pamoja na kuihakikishia Tanzania dhamira ya Uingereza kuendelea kushirikiana na Tanzania katika Sekta za Uwekezaji na Biashara amesema katika bara la Afrika, Tanzania ina nafasi nzuri ya kuvutia uwekezaji kutokana na mshikamano na utulivu wa kisiasa na amani.

error: Content is protected !!