Tanzania yateuliwa kuwa Mjumbe Baraza la Amani na Usalama AU

HomeKimataifa

Tanzania yateuliwa kuwa Mjumbe Baraza la Amani na Usalama AU

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kupitia kanda ya Mashariki kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2022 – 2024.

Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama wapo katika ziara maalum (field mission) nchini Burundi kuanzia tarehe 20 – 22 Juni, 2022 iliyolenga kuangazia hali ya amani na usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Baraza hilo limepongeza kwa maendeleo mazuri yaliyoshuhudiwa nchini Burundi na kwa mchango wake katika kuimarisha hali ya amani na usalama Afrika, hususan Somalia.

Ujumbe wa Baraza hilo ulikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye, ambaye alieleza hali ya amani na usalama nchini humo kuwa imerejea na jumuiya kimataifa imeanza kutambua hilo.

Rais Ndayishimiye alisisitiza kuwa changamoto kubwa barani Afrika kwa sasa ni masuala ya ugaidi ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na changamoto za umasikini, mapinduzi ya Serikali yasiyofuata katiba na ukosefu wa ajira.

Ziara hiyo imetoa nafasi kwa Baraza la Amani na Usalama kufuatilia utekelezaji wa maazimio yake ya nyuma kuhusu Ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa na Baraza la Amani na Usalama Addis Ababa yanazingatiwa.

Mabalozi na wawakilishi kutoka nchi 15 wajumbe wa Baraza hilo walikutana na wadau mbalimbali wa Burundi na Ukanda wa Maziwa Makuu kukusanya taarifa kuhusu hali ya usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo unaongozwa na Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika, Balozi Innocent Shiyo.

 

error: Content is protected !!