√ Ukweli, Upotoshaji na Uhalisia wa Mambo
Na GULATONE MASIGA
Katika siku za karibuni, Kamati Kuu ya Baraza Kuu la CHADEMA ilitoa tamko kuhusu uchaguzi wa Oktoba 29, 2025. Tamko hilo limezua mjadala mpana, lakini baada ya kulichambua kwa kina, imebainika kuwa linatumia hoja za kisiasa zaidi kuliko hoja zenye ushahidi, na lina upungufu mkubwa katika misingi ya kikatiba, kisheria na kiutu.
Makala hii inatoa uchambuzi wa kitaalamu, lakini kwa lugha rahisi kabisa ili kila mtanzania aweze kuelewa ukweli na kutofautisha kati ya hoja na propaganda.
1. Je Uchaguzi Unakuwa Halali kwa Sababu Chama Fulani Kimeshiriki?
La hasha. Katika demokrasia yoyote duniani, uchaguzi unakuwa halali pale tu unapofanyika kwa mujibu wa Katiba na Sheria, sio kwa sababu chama fulani kimeamua kushiriki au kususia. Katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025:-
• Tume ya Uchaguzi ilifuata taratibu za kikatiba,
• Sheria za uchaguzi hazikuvunjwa,
• Vyama 18 vilishiriki kikamilifu na hakuna hata kimoja kilichodai kuonewa.
CHADEMA walichagua kwa hiari yao kutokushiriki uchaguzi; huo ni uamuzi wa chama, si dosari ya mchakato. Kususia uchaguzi ni demokrasia pia.
Kwa hiyo hoja ya kwamba “uchaguzi si halali kwa sababu sisi hatukushiriki” haina msingi wa kikatiba, kisheria wala mantiki ya kisiasa.
2. Je, CHADEMA Walizuiwa Kushiriki Uchaguzi?
Hakuna Ushahidi. Katika tamko lao, CHADEMA hawakuonesha:-
• Zuio la mahakama,
• Amri ya Tume ya Uchaguzi,
• Wala sababu yoyote ya kisheria kuzuia ushiriki wao.
Hakuna taasisi yoyote iliyoizuia CHADEMA kushiriki uchaguzi. Kususia uchaguzi ni uamuzi wao wenyewe na haiwezi kuwa msingi wa kutangaza uchaguzi ni batili au Nchi ina mgogoro wa kisheria na kikatiba.
Chama cha siasa kususia uchaguzi ni sawa na timu kukataa kuingia uwanjani halafu ikadai kuwa mechi ni batili. Haiwezekani.
3. Madai Mazito Bila Ushahidi: Hatari kwa Taifa
Waraka huo umejaa madai makubwa na yenye uzito mkubwa sana, kama vifo vya watu zaidi ya 2,000, mamia ya watu kutekwa, ukatili wa dola na udhibiti wa vyombo vya habari.
Hata hivyo tamko hilo limekosa udhibitisho au ushahidi usioacha shaka ikiwemo ripoti ya uchunguzi na takwimu toka chanzo chenye kuaminika kama vile serikali, tume ya uchunguzi au taasisi yenye kuaminika.
Katika masuala mazito kama vifo, ushahidi ndiyo msingi wa hoja. Kukosekana kwake kunazifanya taarifa hizo kuwa propaganda, ambazo zinaweza kuchochea chuki, taharuki, hofu na migawanyiko bila sababu.
Tukumbushane kuwa Vyama vya siasa vina wajibu wa kuzungumza ukweli, kujenga umoja, na kulinda maslahi mapana ya nchi si kueneza hofu bila uthibitisho.
4. Kuhusu Kukamatwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa
Tamko la CHADEMA limejaribu kuunganisha kukamatwa kwa Mwenyekiti wao, Ndugu Tundu Antipas Lissu, na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Lakini ukweli ni kwamba anakabiliwa na tuhuma za kijinai na suala lake lipo mahakamani.
Ni makosa kwa chama chochote kujaribu kutoa tafsiri ya kisiasa juu ya mambo yaliyoko katika vyombo vya uchunguzi au mahakamani, kwa sababu katika utawala wa sheria hakuna mtu aliye juu ya sheria, awe mwanasiasa ama raia wa kawaida. Mahakama inapaswa kuachiwa itekeleze majukumu yake kwa uhuru bila shinikizo la kisiasa.
5. Pendekezo la ‘Serikali ya Mpito’ Ni Kinyume Cha Sheria naKatiba
CHADEMA wanapendekeza kuundwa kwa ‘Serikali ya Mpito’ isiyoongozwa na Rais aliyepo madarakani Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan bali iongozwe na taasisi za kimataifa.
Hii ni hoja isiyowezekana kwa sababu haisomeki popote kisheria wala haitekelezeki kikatiba.
• Katiba ya Tanzania haitambui serikali ya mpito katika mazingira ya uchaguzi kususiwa,
• Hakuna sheria inayotoa mamlaka kwa taasisi za nje kuongoza nchi,
• Tanzania ni nchi huru, yenye mamlaka kamili ya ndani,
• na taasisi/shirika/wakala wowote wa nje hana haki ya kusimamia madaraka ya wananchi ndani ya Tanzania.
Pendekezo hili linapingana moja kwa moja na misingi ya uhuru wa taifa na Katiba yetu.
MWISHO
Tuongee Ukweli, Tuilinde Tanzania
Baada ya kufanya uchambuzi wa kina, imekuwa wazi kwamba tamko la CHADEMA:-
• Linakosa ushahidi,
• Linapingana na Katiba,
• Linalenga kumuondolea uhalali na ushawishi wa Kisiasa Rais aliyopo Madarakani Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa tuhuma zisizo na mashiko wala uhalali wowote wa kisiasa, kisheria na kikatiba.
• Linatumia lugha ya hisia,
• Linaeneza hofu isiyo na msingi,
• Linalenga kutia doa heshima ya Tanzania kimataifa
• na Linalenga kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi za nchi bila sababu.
Hivyo ni muhimu kwa serikali, vyama vya siasa, watanzania wote na wadau wa demokrasia kuendelea kuheshimu Katiba, kutetea amani na umoja, kuepuka propaganda na kuweka mbele maslahi mapana ya Taifa.
Si busara kupeleka nje ya nchi taswira ya kwamba Tanzania ni Taifa linalovurugika wakati ukweli ni tofauti. Mijadala ya kisiasa ni muhimu, lakini lazima iwe ya ukweli, iheshimu tunu za Taifa, iwe ya hoja na ushahidi si ya mihemko na vitisho dhidi ya utulivu na usalama wa Nchi.
Katika wakati huu, Watanzania tunahitaji uongozi, umoja, na sauti za kuijenga Tanzania, si kuibomoa.
Kwa Maoni Na Ushauri
0768497974


