Mamlaka ya reli Tanzania na Zambia (TAZARA) imeelezea kushtuka kutokana na kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya maiti za watu waliouwawa na watu wasiojulikana kutupwa relini ili ionekane wamegongwa na treni. Kufuatia hali hiyo TAZARA imeiomba serikali mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa kina na kubaini chanzo cha mauaji hayo.
Mhandisi wa Ishara na mawasiliano wa Wilaya ya kitazara Mbeya Betwel Kamugisha amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba kuwa “Reli ya TAZARA inapita katika mikoa mitatu ya Njombe, Mbeya na Songwe kwa upande wa Wilaya ya Mbeya kitazara, kwa hiyo matukio ya maiti kutupwa relini mara kwa mara huwa yanatokea maeneo tofauti katika mikoa hii”’
“Kuna muda mwingine mnakuta mwili wa mtu umegongwa na treni, lakini kuna maiti nyingine zinaonekana kabisa mtu aliuawa na watu wasiojulikana na kuja kutupwa relini ili aonekane kagongwa na treni. Sasa nimewasilisha changamoto hii ili Mkuu wa Mkoa naye aweze kuiwasilisha kwenye kamati yake ya ulinzi na usalama ili waone namna gani wanaweza kufanya uchunguzi matukio hayo yaweze kukoma”.