Shirika la Reli Tanzania (TRC) limekamilisha majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo yaliyowasili nchini Desemba 2024. Majaribio ya mabehewa hayo yaliyochukua mwezi mmoja yalifanyika chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA). Lengo la majaribio hayo yalikuwa ni kuangalia umadhubuti wa mabehewa treni inapokuwa kwenye mwendo.

Mabehewa ya mizigo ya SGR
LATRA imefanya ukaguzi wa mabehewa yote 264 kati ya hayo 200 yakiwa ni ya makasha (containers carriers) na 64 ni ya mizigo isiyofungwa (loose cargoes). Katika hatua nyingine LATRA imesema itatoa ithibati kwa TRC, kama Sheria na Kanuni zinavyoeleza ili mabehewa yaanze kubea na kusafirisha mizigo.
Kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 kati ya 1,430 yanayotengenezwa na kampuni ya CRRC ya China, ni kiashiria kuwa usafirishaji mizigo katika reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) uko mbioni kuanza.