Uandikishaji daftari la wapiga kura wafikia asilimia 94.8 ya lengo

HomeKitaifa

Uandikishaji daftari la wapiga kura wafikia asilimia 94.8 ya lengo

Serikali imesema Watanzania milioni 31.2 sawa na asilimia 94.8 ya lengo wamejitokeza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024.

Zoezi la kujiandikisha katika daftari la kupiga kura la Serikali za Mitaa limefanyika kwa siku 10 nchi nzima kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu na kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kujiandikisha tayari kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo.

Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 21, 2024 amesema matokeo hayo yamechangiwa na uhamasishaji pamoja na utolewaji wa elimu uliofanywa na wizara hiyo.

“Mafanikio haya yamechagizwa na uwekezaji mkubwa wa uelimishaji na uhamasishaji katika ngazi zote muhimu ambazo Tamisemi inasimamia…

….Nawapongeza Watanzania waliojitokeza kujiandikisha kwa kuwa tayari wameshapata sifa ya kisheria ya kutekeleza haki ya kikatiba ya kuchaguliwa na kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa wanaowataka wenyewe,” amesema Mchengerwa.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo lengo la Serikali lilikuwa ni kuandikisha Watanzania milioni 32.9 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambao wanaruhusiwa kupiga kura.

Mpaka kufungwa kwa zoezi hilo Oktoba 20 mwaka huu Watanzania milioni 31.2 walijiandikisha kati yao wanaume walikuwa milioni 15.2 sawa na asilimia 48.7 na wanawake ni milioni 16.04 sawa na asilimia 51.29.

Tamisemi imebainisha kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji orodha ya wapiga kura itabandikwa kuanzia leo katika sehemu za matangazo kwenye vijiji na mitaa ili kuwezesha wananchi kukagua orodha hiyo ili kuomba kurekebisha majina, kubadilisha taarifa zilizopo katika orodha hiyo au kufuta jina ikiwa aliyeorodheshwa amefariki.

Ukaguzi na uhakiki huo utafanyika kwa siku saba kuanzia leo Oktoba 21 hadi Oktoba 27 nchi nzima ikifuatiwa na zoezi la wagombea kujiandikisha kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba Mosi mwaka huu.

“Napenda kutoa rai kwa wananchi wenye sifa za kuchaguliwa kuwa viongozi ajitokeze kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi Novemba 1, 2024 ili kutimiza haki yao ya kikatiba, kisheria na kikanunui kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi unakuja,” ameongeza Mchengerwa.

Aidha, Mchengerwa amewataka wasimamizi wa uchaguzi pamoja na vyama vya siasa na vyombo vya dola kudumisha amani katika kipindi chote ambacho mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakuwa unafanyika.

“Nitoe rai kwa vyama vyote fya siasa viendelee kuwasihi wanachama wao kuendelea kudumisha amani na utulivu katika maeneo yetu, niwasihi wananchi vyama vyote kufuata Sheria, kanuni, muongozo ya uchaguzi ili kulinda amani utulivu na ustawi wa nchi yetu,” amesema Mchengerwa.

error: Content is protected !!