Serikali imesema miradi inayotarajiwa kuanza utekelezaji mwaka 2025 ni ujenzi wa barabara ya haraka kutoka Kibaha hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 78.9.
Mingine ni wa ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto chini ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi, mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) chini ya Dart na mradi wa ujenzi wa jengo la biashara na hoteli ya nyota nne katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Miradi hiyo itatekelezwa kwa uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ili kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na huduma.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo wakati akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania leo Desemba 31, 2024 akieleza mpaka sasa kuna miradi 74 ya ubia iliyopo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji.