Kati ya vitu vinavyosababisha wengi kukosa kazi ni barua mbaya ya utangulizi na wengine huandika hadi waraka wa Petro kwa mwajiri wakidhani kuwa ndio njia rahisi ya kupata kazi.
Ukweli ni kwamba mwajiri ana barua nyingi za kusoma hawezi kusoma barua yako ya kurasa mbili ndio maana kukawa na CV. Barua ya kuombea kazi hukusaidia kujitambulisha kwa ufupi na kuelezea ambayo hayapo kwenye CV.
Anuani yako upande wa kulia juu kabisa ni muhimu sana kwenye kuandika barua. Anuani hiyo iwe na Jina lako, sanduku la posta, mkoa unapotoka, tarehe, namba ya simu na barua pepe.
Ruka mstari mmoja kisha anza aya mpya kushoto yenye anuani ya mwajiri
Ruka tena mstari mmoja kisha tanguliza salamu zako (Dear Sir/ Madam,) kama hujui jinsia ya mwajiri au kama ni Taasisi. Lakini kama unamjua mwajiri basi mtaje jina au onesha jinsia yake (Dear Mr. Juma; au Dear Sir;).
Kinachofuata ni kichwa cha barua yako. Muhimu usipigie mstari kichwa cha barua kama utaweka bold. Kwa fano unaweza kutumia YAH: MAOMBI YA NAFASI YA UDEREVA II TRA au YAH: MAOMBI YA NAFASI YA UDEREVA II TRA na siyo YAH: MAOMBI YA NAFASI YA UDEREVA II TRA usimfokee mwajiri.
Sasa kuja kwenye kiini cha barua yenyewe haya ndio ya muhimu.
Aya ya kwanza; Husika na kichwa cha habari hapo juu/ kichwa cha habari tajwa (mstari 1)
Aya ya pili elezea kuwa unafanya maombi ya kazi tajwa kwenye kampuni yenu (itaje jina) kama ilivyotangazwa kwenye tovuti/mtandao wa… na nini likikusukuma kufanya maombi. (mistari 2)
Katika aya ya tatu utaelezea sifa zinazokufanya wewe ufanye kwenye nafasi hiyo kwa kuzingatia vigezo vyao walivyotangaza. Kwa mfano; Kwa uzoefu niliojipatia ndani ya miaka saba ya kufanya kazi kama dereva katika kampuni nne tofauti (Kampuni hizi nne utazitaja kwa majina kwenye CV yako) pamoja na kuendesha viongozi mbalimbali ikiwemo wabunge na mawaziri imenijengea umakini kwenye kazi yangu na uwezo wa kufanya kazi na watu wa hulka, haiba na umri tofauti tofauti kwenye mazingira ya mjini, vijijini na porini. (mistari 3 -5)
Hapa sasa unaanza kwa kuelezea ujuzi mwingine ulionao nje ya udereva na mafanikio ama tuzo mbalimbali ulizowahi kupata na unajishughulisha na nini kwa wakati huu. Eleza pia namna unavyopanga kutekeleza majukumu yako pale utakapopata kazi kwa kutumia ujuzi wako. (mistari 3-5)
Funga kwa kushukuru kwa nafasi hiyo uliyopata na kwa kujiamini malizia kwa kuwahakikishia kuwa wewe unafaa kwa nafasi hiyo na kuwaomba wasome zaidi kwenye CV yako.
hatua ya mwisho ni kutia saini barua ikifuatiwa na jina chini yake.
_________________
Juma Msukuma