Wataalamu wa wanyamapori katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika (Mweka) wamepongeza uamuzi wa serikali kuweka mipaka ya eneo la Pori Tengefu la Loliondo( LGCA).
Mkuu wa chuo hicho kilichopo Moshi, Profesa Jafari Kideghesho amesema hatua hiyo ni mojawapo ya njia tatu zinazojumuisha uboreshaji wa eneo tengefu, mchakato wa kushusha hadhi au utoaji wa gazeti (PADDD) na si jambo geni katika mizunguko ya ikolojia yenye lengo la kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500.
“Hii ni sababu ya misngi ya kuokoa mfumo wa ikolojia Serengeti-Ngorongoro kutokana na kuwa katika hatari ya kutoweka,”
“Kupungua kwa ukubwa wa eneo la hifadhi kupitia mabadiliko ya mipaka halali ni muhimu katika kulinusuru eneo hilo ambalo limeathiriwa vibaya ba shughuli za kibinadamu ikiwamo ufugaji na ongezeko la mifugo,”
“Endapo hatutapunguza shughuli za kibinadamu katika maeneo haya, basi kuna uwezekano kwamba uzuri wa Ngorongoro na Serengeti ukapotea siku za usoni,” alisema Profesa Kideghesho.
Serikali imeanza kuweka mipaka ya eneo hilo kwa madhumuni ya kuweka uwiano sahihi kati ya uhifadhi na maeneo ya watu.
Utaratibu huo utahusisha kilomita za mraba 2,500 ambazo zitatengwa kwa shughuli za kibinadamu na kilometa 1,500 kubakia kuwa eneo la hifadhi.