Rais Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuanza kutekeleza kikamilifu sera bora za kilimo zilizowekwa na jumuiya hiyo ili kuepukana na upungufu wa chakula unaowakabili takribani watu milioni 51.3.
Kwa mujibu wa Rais Samia, upungufu wa chakula katika nchi za SADC umeongezeka kwa asilimia 25.7 kati ya mwaka 2019/20 na 2020/21.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa 53 wa jukwaa la mabunge ya nchi za SADC jana Julai 3, 2023, amewaambia washiriki kuwa eneo lenye jumla ya kilomita za mraba milioni 9.8 linalofaa kwa kilimo katika nchi za SADC linaweza kuilisha Afrika kukiwa na usimamizi thabiti na utekelezaji wa sera bora za kilimo.
“Watu wanaokabiliwa na upungufu wa chakula wameongezeka kwa asilimia 25.7 kwa mwaka mmoja hii haikubaliki…bado tuna kilomita za mraba milioni 9.8 zinazoweza kulilisha bara la Afrika na zaidi, ikiwa zitatumika ipasavyo.,” amesema Rais Samia jijini Arusha.
Rais Samia amesisitiza kuwa huu ni muda muafaka wa kuanza utekelezaji wa sera na programu ambazo zimekuwa zikiasisiwa bila kufanyiwa kazi ikiwemo Sera ya Kilimo ya SADC ya mwaka 2014.
Sera hiyo inabainisha kuwa nchi za SADC zinapaswa kutenga asilimia 10 ya bajeti za nchi zao kwa ajili ya shughuli za kilimo jambo ambalo bado halijaanza kutekelezwa kikamilifu katika nchi nyingi za jumuiya hiyo.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza sekta ya kilimo imepata msukumo mpya nchini Tanzania ambapo bajeti ya kilimo imefikia zaidi ya Sh970 bilioni kwa mwaka 2023/24 ambapo asilimia 84 ikienda kwenye miradi ya maendeleo.
Kiwango cha fedha katika bajeti ya mwaka 2023/24 kimeongezeka kwa Sh219.6 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 29 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita.