Serikali ya Tanzania imeendelea na juhudi zake za kuimarisha ushirikiano na nchi jirani ikiwemo Burundi ambapo pamoja na mambo mengine imekusudia kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo.
Waziri wa kilimo, Prof. Adolf Mkenda amefanya ziara ya kikazi ya siku 2 nchini Burundi kuanzia tarehe 18 Oktoba 2021 ambapo pamoja na mambo mengine katika ziara hiyo Waziri Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Dkt Rurema Deo-Guide ambapo kwa kauli moja wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta ya Kilimo.
Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Ngozi na Kayanza alipotembelea kujionea mashamba ya kilimo cha mahindi (Block Farming) pamoja na kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya nchini Burundi ya Isabu, Waziri Mkenda amesema kuwa lengo la ziara yake katika maeneo hayo ilikuwa ni kujionea hali ya ubora wa mazao ya wakulima yanayotumia mbolea ya FOMI.
“Tumekutana na wanasayansi wa hapa Burundi ili kuzungumza nao waweze kutueleza kuhusu utafiti walioufanya wa mbolea ya FOMI ili kujiridhisha kabla ya kuingia makubaliano ya kuanza matumizi ya mbolea hiyo kule nchini kwetu” Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amemuhakikishia mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Dkt Rurema Deo-Guide kuwa atampatia mualiko ili aweze kutembelea Tanzania kwa ajili ya kujifunza kuhusu kilimo cha mazao mbalimbali na kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.