Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam umeonyesha mafanikio makubwa, na kuleta mabadiliko chanya katika uchumi wa taifa. Kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Limited zimeendelea kuendesha baadhi ya maeneo ya bandari hiyo, na matokeo yake ni ya kuridhisha.
Kwa mujibu wa ripoti za mapato ya forodha, kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025 kimeonyesha ongezeko kubwa la mapato, ambapo jumla ya shilingi trilioni 8.26 zimekusanywa, ikilinganishwa na shilingi trilioni 7.08 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2023/2024, kabla ya ushirikishwaji wa waendeshaji binafsi. Hii ni ongezeko la shilingi trilioni 1.18.
Aidha, gharama za uendeshaji wa bandari zimepungua kwa asilimia 30, kutoka shilingi bilioni 775.01 hadi shilingi bilioni 685.16, na kuleta ufanisi mkubwa katika usimamizi wa rasilimali. Mabadiliko mengine yanayoonekana ni kupungua kwa muda wa kusubiri meli, ambapo meli za mizigo zinazochukua zaidi ya wiki 6 sasa zinasubiri kwa wastani wa siku 7 tu. Vilevile, meli za makasha gatini sasa husubiri kwa wastani wa siku 3 tu, kutoka wastani wa siku 10 kabla ya ushirikishwaji.
Mabadiliko haya yanaonekana pia katika ufanisi wa huduma kwa wateja, ambapo wastani wa makasha ya shehena yanayohudumiwa kwa mwezi umeongezeka kutoka 17,000 hadi 25,000, sawa na ongezeko la asilimia 47.
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza katika maboresho ya miundombinu ya bandari ili kuongeza tija na kuendeleza uchumi wa taifa. Ushirikishwaji huu wa sekta binafsi umeonekana kuwa moja ya mikakati muhimu katika kufanikisha malengo haya.