Vijana 100 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamepewa msaada wa nguruwe 100 na halmashauri hiyo ikishirikiana na mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM) ambapo fedha zaidi ya Sh. milioni 14 zimetumika kuwasaidia vijana hao wanaotoka kwenye mazingira magumu.
Meneja wa Miradi ya YAM, Zilipa Mgeni alisema taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza mradi wa kuwasaidia vijana kwenye vijiji 16 vya kata za Luhunga, Ihanu na Mdabul walengwa wakuu wakiwa vijana wanaotoka katika mazingira magumu, wakiwamo waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Mgeni alieleza kwamba kila kijana ambaye nimnufaika na mradi huo amepatiwa nguruwe wawili,dume na jike pamoja na chakula cha mwezi mmoja wa mwanzo.
Mmoja wa wanufaika hao, Felix Kitinusa amesema msaada huo ni ukombozi mkubwa kwake kwa kuwa alikuwa akitamani kuwa mfugaji wa nguruwe,lakini kikwazo kikubwa kilikuwa elimu na mtaji wa kuendesha shughuli hiyo.