Baada ya miaka tisa bila kupandishwa, Serikali ya Awamu ya Sita imetangaza viwango vipya vya mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.
Hata hivyo wataalamu wa uchumi wamesema viwango hivyo vipya vya kima cha chini cha mshahara, vitakuwa na matokeo chanya na hasi, wakisema ingawa mapato ya Serikali yataongezeka, lakini mfumuko wa bei nao utapanda.
Kima hicho cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kimetangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako kupitia tangazo la Serikali (GN) namba 697 la Novemba 25,2022.
Hata hivyo, amri hiyo ya Serikali itakayojulikana kama amri ya kima cha chini cha mshahara kwa mwaka 2022 itaanza kutumika Januari 1,2023 na kwamba amri kama hiyo ya kima cha chini kwa sekta binafsi iliyotolewa mwaka 2012 imefutwa.
Kima hicho cha chini kimegusa takribani sekta 12 ambazo ni kilimo, afya, mawasiliano, kazi za majumbani na hotelini, huduma za ulinzi binafsi, nishati, usafirishaji, ujenzi , madini, shule binafsi na sekta ya biashara na viwanda.