Wabunge wampongeza Rais Samia kwa ubunifu na mageuzi katika Sekta ya Utalii

HomeKitaifa

Wabunge wampongeza Rais Samia kwa ubunifu na mageuzi katika Sekta ya Utalii

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu alioufanya kwenye sekta ya utalii kupitia filamu ya Tanzania the Royal tour na Amaizing Tanzania ambazo zimechangia kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya utalii kutoka watalii 1,711,625 mwaka 2021 hadi watalii 5,360,247 mwaka 2024.

Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Mhe. Joseph Msukuma, akichangia hotuba hiyo ameeleza kuwa Rais Samia kupitia Filamu ya Tanzania the Royal tour imeonyesha ubunifu wa hali ya juu na kuleta faida ya kuongeza mapato na idadi ya watalii na kusisitiza kuwa Serikali iendelee kubuni mawazo na mbinu mpya za kuendeleza sekta ya utalii.

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Tabora Mhe. Hawa Mwaifunga amebainisha kuwa baada ya Filamu ya Royal tour kufanya vizuri, Wizara ya Maliasili na utalii inapaswa kuja na mkakati mwingine wa kutangaza vivutio vya utalii ukiwemo kutumia fursa ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2027

Mbunge wa Makete Mhe. Festo Sanga ameishauri Serikali kuendelea kutatua changamoto katika maeneo ya hifadhi pamoja na kutumia mapato yanayopatikana kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi, kuboresha miundombinu ya uhifadhi na kutangaza utalii katika masoko ya kimkakati.

Naye Mhe. Mrisho Gambo mbunge wa Arusha mjini amependekeza Serikali kuziwezesha taasisi za Uhifadhi kukusanya maduhuli ya shughuli za utalii ili ziweze kukarabati miundombinu ya utalii kwa wakati na taasisi hizo zichangie mapato serikalini kupitia mfumo wa gawio. Aidha ameishauri tozo za shughuli za utalii ikiwemo matumizi ya fedha za kigeni kwenye sekta ya utalii kuendelea kuboreshwa kwa kushirikiana na wadau wa utalii.

error: Content is protected !!