Wafahamu Marais 5 wa Afrika waliouawa wakiwa madarakani

HomeKimataifa

Wafahamu Marais 5 wa Afrika waliouawa wakiwa madarakani

Matukio ya kuuawa kwa viongozi wa juu wa nchi duniani yamekuwa yakipingua kasi katika miongo ya hivi karibuni, lakini hata kwa uchache wake bado yanatokea.

Kifo cha hivi karibuni cha  Rais wa Haiti Jovenel Moïse aliyeuawa kwa kushambuliwa kwa risasi akiwa kwenye makazi yake, katika mji mkuu, Port-au-Prince ni mfano mmoja tu wa viongozi wakuu wa nchi zaidi ya 100 kuuawa katika kipindi cha miongo 10 iliyopita.

Ripoti moja iliyochapishwa mwaka 1998 nchini Marekani ya Military Medicine (Vol. 163), inaonesha kati ya mwaka 1965 mpaka 1996 viongozi wakuu wa nchi 261 walifariki, kati yao viongozi 118 walifariki wakiwa madarakani huku asilimia 44% ya viongozi hao waliuawa.

Kati ya Viongozi 144 waliofariki baada ya kutoka madarakani, asilimia 11% waliuawa.

Matukio ya kuuawa kwa viongozi hao yanatokea duniani kote, lakini mara nyingi zaidi hutokea katika nchi za masharki ya kati, Asia ya Kusini na nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Ukiacha viongozi wengi huko nyuma kama John Kennedy wa Marekani, Park Chung-hee wa Korea Kusini, Francois Tombalbaye wa Chad, Hafizullah Amin wa Afghanistan, Anwar Sadat wa Misri na Thomas Sankara wa Burkina Faso, BBC inakuletea baadhi tu ya marais hasa kutoka Afrika ambao waliouawa kwa kushambuliwa kwa risasi wakiwa madarakani.

1: Idriss Deby – Chad

Kifo cha Rais Deby kilitokea siku moja tu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa 2021, akipata asilimia 80% ya kura zote katika uchaguzi huo wa April 11, 2021.Deby aliiongoza Chad kwa miaka 30 mpaka Aprili 2021, alipouawa wakati akiongoza majeshi ya nchi hiyo kukabiliana na waasi waliokuwa wanataka kumuondoa madarakani.

Deby aliingia madarakani kwa mapinduzi na kumfurusha aliyekuwa Rais na mkubwa wake jeshini, Hissene Habre. Hata hivyo uhusiano wao ulianza kuyumba mapema tu baada ya Habre kumtuhumu Deby kutaka kumpindua. Deby akatimkia Libya baadae Iraq alipokusanya nguvu na kurudi nchini Chad mwaka 1989 na kumfurusha Habre.
Hata hivyo uasi kwa mika kenda na kenda unaitafuna Chad, ambayo ni moja ya nchi masikini kabisa duniani, ambapo zaidi ya nusu ya watu wake milioni 15.8 wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa.

Kulikuwa na vikundi vya waasi vilivyoendesha mapigano ya kumuondoa madarakani Deby, ambavyo vilifanikiwa kumchapa risasi walipoukaribia mji wa Djamena na kumjeruhi kabla ya kupoteza maisha.

2: Sheikh Abeid Aman Karume – Zanzibar

Alikuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar na makamu wa kwanza wa Rais wa Tanzania. Anaheshimika sana visiwani humo kwa jitihada zake za kuileta Zanzibar pamoja, lakini pia kuviunganisha visiwa hivyo na Tanganyika na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania.Sheikh Karume aliuawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi (ASP) visiwani mjini Zanzibar mnamo tarehe 7 Aprili, 1972.

Anatajwa mmoja wa walinzi wake kufanya shambulio hilo ingawa hakuna uhakika wa hilo mpaka leo, kutokana na kutowekwa wazi kwa taarifa rasmi ya kifo cha kiongozi huyo ambaye hawezi kusahaulika katika historia ya ukombozi wa visiwani humo kutokana na misingi aliyowajengea Wazanzibar.

3: Muammar Gaddafi – Libya


Anakumbukwa kwa ubabe wake wa vita uliomsaidia kuingia madarakani mwaka 1969. Alikamatwa na kuteswa kiasi kabla ya kuuawa Oktoba 20,2011, kufuatia mapigano yaliyoitwa ’Battle of Sirte, kati ya wanajeshi wanaomtii na wanajeshi wa NTC wasiomtii kiongozi huyo.

Alikutwa amejificha kwenye kalavati dogo kuwakwepa wanajeshi hao. Zilisambaa video zikiwaonyesha waasi wa NTC wakimpiga kiongozi huyo ambao baadae walimmaliza kwa kumpiga risasi kadhaa. Baade kukaja ripoti ambayo haijathibitishwa kwamba alijiua mwenyewe kwa bastola yake. Ripoti inayopingwa na waliokuwa walinzi wake.Mwili wake ulihifadhiwa kwenye jokofu maalumu na kwa siku kadhaa ili kuwapa nafasi raia washuhudie kwamba kiongozi huyo hayuko hai tena.

4: Laurent-Desire Kabila – DR Congo


likuwa Rais wa tatu wa DR Congo wakati huo inaitwa Zaire. Aliongoza nchi hiyo kuanzia mwaka Mwaka 1997 mpaka alipouawa Januari mwaka 2001. Baada ya kuingia madarakani kwa kumfurusha Mobutu Seseseko, Kabila alibadilisha katiba na kurejesha jina la DRC na kulifuta jina la Zaire.

Alipigwa risasi ofisini kwake Januari 16, 2001 na kukimbizwa Zimbabwe kwa matibabu. Kifo chake kilitangazwa January 18, ingawa Waziri wa afya wa wakati huo, Leonard Mamba aliyekuwa chumba cha pili cha ofisi wakati shambulio likitekelezwa alieleza kwamba Kabila alifariki papo hapo.

Wiki moja baadae mwili wake ulirejeshwa DRC kwa ajili ya mazishi ya kitaifa, kabla ya mtoto wake Joseph Kabila kumrithi na kuwa Rais wa nchi hiyo siku 10 tu tangu baba yake Kabila auawe.
Zaidi ya watu 130 walihusishwa na njama za kifo chake akiwemo mmoja wa wapwa zake na kuhukumiwa adhabu mbalimbali.

5. João Bernardo Vieira – Guinea Bissau


Vieira aliongoza Guinea-Bissau kwa vipindi vitatu tofauti, alianza mwaka 1980 mpaka1984, akaendelea kipindi cha pili 1984 mpaka 1999, na kipindi cha tatu ilikuwa mwaka 2005 mpaka 2009. Baada ya kuingia madarakani mwaka 1980, Vieira aliiongoza Guinea-Bissau kwa miaka 19 mna akashinda uchaguzi mkuu wa vyama vingi wa mwaka 1994.

Hata hivyo vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1998-1999 vilisitisha utawala wake na kutimkia ng’ambo. Akarejea kwenye siasa mwaka 2005 na kushinda uchaguzi wa rais. Hata hivyo miaka mine baadae (Machi 2, 2009) akauawa na wanajeshi wake , masaa machache baada ya kuuawa kwa mkuu wa majeshi Jenerali Batsta Tagme Na Waie. Ripoti za kifo chake haziko wazi sana, wapo wanaoamini kauawa kwa bomu na wengine kauawa kwa risasi na baadae bomu.

Chanzo: BBCSwahili

error: Content is protected !!