Jamii ya Wahadzabe iliyopo katika eneo la Yaeda Chini jana wamekabidhiwa kitoweo cha nyama pori aina ya Nyumbu na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere ikiwa ni takwa la jamii hiyo kupewa kitoweo cha nyamapori ili kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ambayo inayofanyika leo Agosti 23,2022.
Licha ya Kiongozi wa Kimila wa Jamii ya Hadzabe, Athuman Mangula kuishukuru Serikali kwa kuwapa kitoweo hicho lakini amebainisha kwamba awali takwa la jamii hiyo ilikuwa ni kupewa Mbuni na Serikali na badala yake wamepewa Nyumbu na kueleza kuwa manyoya ya Mbuni hutumika kufanyika mila kama tiba endapo wakipata ugonjwa.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere amesema kwamba ombi hilo limepokelewa na litafanyiwa kazi.
Ikumbukwe kuwa jamii hiyo ya Hadzabe ni miongoni mwa makabila adimu na adhimu yanayoendeleza mila na tamaduni za asili, miongoni mwa tamaduni hizo ni uwindaji, ulaji wa matunda pori, ulaji wa asali pamoja na maisha ya kuhama.
Jumla ya nyumbu 20 wametolewa bure na Serikali kwenye jamii ya Hadzabe kwa minajili ya ushiriki wa Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23.