Serikali imewapangia vituo vya kazi waajiriwa wapya 18,449 kati ya 21,200 ambao ajira zao zilitangazwa wa kada za ualimu na afya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, Angellah Kairuki alisema hayo Dodoma jana wakati wa kutangaza upangaji wa vituo vya kazi kwa waombaji.
Kairuki alisema maombi 171,916 yamepokelewa na kati ya hayo wa kada za afya ni 48,705 na kada ya ualim ni 123,211.
Uhakiki
Kairuki alisema uhakiki wa awali wa kimfumo uliofanywa katika maombi 171,916 yaliyopokelewa, waombaji 49,089 waliondolewa kwenye mchakato na hivyo kubaki na waombaji 122,827.
Waombaji waliondolewa awali 1,456 waliomba nafasi ya ualimu wakiwa wamehitimu kabla ya mwaka 2015 na waombaji 47,633 waliomba masomo ambayo hayakutangazwa.
Uhakiki wa pili uliohusisha nyaraka, waombaji 36,065 kati ya 122,827 walovuka uhakiki wa kwanza waliondolewa kwenye mchakato na hivyo kubaki na waombaji waliokidhi vigezo 86,448.
“Walioondolewa awamu hii ni kutokana na kutoambatanisha baadhi ya vyeti vya kitaaluma, kudanganya mwaka wa kuhitimu, kutokuwa na leseni za kitaauma, kutowasilisha cheti cha kuzaliwa na kudanganya kuwa ni walemavu,” alisema.
Kairuki alisema katika uhakiki huo waombaji 56 waliwasilisha vyeti vya kughushi na waombaji 50 vyeti vyao vilikuwa vinatumika na waajiriwa wengine.