Madaktari wanaotibu magonjwa ya afya ya akili, wameiomba serikali kupitia upya sheria inayowafunga watu wanaofanya jaribio la kujiua ili wapatiwe tiba na kuondoa tatizo hilo kwa jamii.
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Huduma ya Ubora wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe, Dk. Minael Urio, alitoa rai hiyo juzi baada ya hitimisho la matembezi ya hisani ya kupinga kujiua.
Alisema, waathirika hao wanapaswa kupelekwa hospitalini kupata matibabu ili kubaini tatizo linalowasumbua mpaka kufikia hatua ya kutaka kujiua.
“Wakipata nafasi ya kutibiwa, inaweza kusaidia kumtoa katika hatua aliyofikia badala ya kubaki vivyo hivyo akiwa mahabusu. Tunaomba sheria iangaliwe upya ili kuwanusuru waathirika wa matukio haya nchini,” alishauri.