Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) leo limetangaza matokeo ya mtihani ya kidato cha sita kwa mwaka 2023 huku ufaulu wa jumla kwa watahiniwa wa shule ukiongezeka kidogo kwa asilimia 0.03 kulinganisha na mwaka 2022.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Ally Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo ya kidato cha sita na ualimu kwa mwaka 2023 leo Julai 13, 2023 amesema ufaulu wa jumla umeongezeka hadi asilimia 99.9 mwaka huu kutoka asilimia 99.8 mwaka jana.
“Jumla ya wanafunzi 96,010 sawa na asilimia 99.9 ya waliosajiliwa wamefaulu mtihani wa kidato cha sita (ACSS) mwaka 2023 ambapo ufaulu umeongezeka kidogo kulinganisha na ule wa mwaka 2022,” amesema Dk. Mohamed.
Kwa mwaka 2023 wanafunzi 160,883 walisajiliwa kufanya mtihaniwa kuhitimu kidato cha sita wakiwemo watahiniwa wa shule 96,858 ambapo ni watahiniwa 105,577 ndio walifanya mtihani huo.
Ubora wa ufaulu waongezeka
Necta wamebainisha kuwa ubora wa ufaulu nao umeongezeka kufuatia idadi kubwa ya watahiniwa kupata daraja la kwanza hadi la tatu ambapo zaidi ya asilimia 80 wamepata daraja la kwanza na la pili.
“Watahiniwa 95,442 sawa na asilimia 99.3 wamefaulu vizuri, daraja la kwanza hadi la tatu, waliopata daraja la kwanza ni 36,527 sawa na asilimia 38, daraja la pili ni 44,312 ambao ni sawa na asilimia 46 hivyo kwa daraja la kwanza na la pili tuna watahiniwa 80,839 sawa na asilimia 88,” amesema Mohamed jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mohamed mwaka 2022 watahiniwa waliofaulu daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 83,877 sawa na asilimia 99.24 hivyo ubora ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.06
Wavulana wakimbiza
Mohamed amebainisha kuwa wastani wa ufaulu unaonesha wavulana wamefanya vizuri zaidi kuliko wasichana kwa mwaka 2023 ambapo ubora wa ufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu ni mzuri zaidi kwa wavulana kwa asilimia 0.12
Kwa daraja la kwanza pekee wavulana wamefaulu kwa asilimia 41 huku wasichana wakifaulu kwa asilimia 35.