Matokeo kidato cha sita 2023, 11 wafutiwa

HomeKitaifa

Matokeo kidato cha sita 2023, 11 wafutiwa

Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 11 wa kidato cha sita baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu katika mtihani uliofanyika Mei mwaka huu wa 2023.

Idadi ya waliofutiwa matokeo mwaka huu imepungua ikilinganishwa na 15 waliofutiwa mwaka jana na 27 waliofutiwa mwaka 2021, jambo linalodhihirisha kuwa vitendo hivyo vilivyo kinyume na Sheria vinadhibitiwa.

“Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 11.  Nane wa shule na watatu wa kujitegemea wa mtihani wa kidato cha sita ambao walibainika kufanya udanganyifu,” amesema  Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Ally Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo ya kidato cha sita na ualimu kwa mwaka 2023 leo Julai 13, 2023.

Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) cha Sheria ya Necta sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu ch 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani mwaka 2016 ambazo zinakataza vitendo vyovyote vya udanganyifu wakati wa mitihani.

Matokeo yaliyozuiliwa  

Necta pia imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 169 wakiwemo 153 wa mtihani kidato cha sita, nane walimu daraja A na nane wa stashahada ya walimu wa sekondari ambao walipata matatizo ya kiafya na hivyo kushindwa kufanya masomo yote au kwa idadi kubwa ya masomo.

“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mitihani kwa masomo ambayo hakufanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka 2024 kwa mujibu wa kifungu cha 30(1) cha Kanuni za Mitihani,” amesema Dk Mohamed.

 

error: Content is protected !!