Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya aunga mkono kauli ya Rais Samia Suluhu

HomeKitaifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya aunga mkono kauli ya Rais Samia Suluhu

Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amekiri kuwa ukosoaji wa hivi majuzi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhusu tabia ya Wakenya huenda una ukweli fulani.

Akizungumza katika mahojiano na Citizen TV jioni ya Jumanne, Mei 20, Mudavadi alijibu kauli ya Suluhu iliyolalamikia ukosefu wa heshima miongoni mwa Wakenya, hususan katika namna wanavyojieleza. Waziri huyo wa Mambo ya Nje alisema kiongozi huyo wa Tanzania hakuwa anakosea kabisa katika maoni yake.

“Nadhani kuna ukweli fulani,” Mudavadi alisema. “Tukubali ukweli. Kiwango cha adabu, kiwango cha matusi ambacho wakati mwingine huonekana kuenea Kenya, kinapita kiasi. Ingawa tuna uhuru wa kujieleza, ukweli kwamba yeye (Suluhu) anasema watu wakati mwingine wanazidi mipaka katika matamshi yao nchini Kenya—ni kweli.

Mudavadi, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri, alibainisha kuwa utamaduni wa Wakenya wa kujieleza kwa uhuru mara nyingi husababisha matamshi yasiyo na ustaarabu, hasa katika mijadala ya kisiasa na kijamii.

“Mimi pia ni Mkenya,” aliendelea. “Na ukweli ni kwamba, namna yetu ya kujieleza na kauli zetu, kwa sababu tuna uhuru wa kusema, wakati mwingine hukosa maadili ya hali ya juu.

Katika uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya 2001 ( Toleo la 2024) uliofanyika tarehe 19 Mei, 2025 Rais Samia aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama na wasimamizi wa Sera za Mambo ya Nje kuwachukulia hatua wanaharakati kutoka nje ya nchi na wa ndani wenye nia ya kuvuruga amani, usalama na utulivu.

error: Content is protected !!