Walemavu wa viungo mkoani Mtwara, wameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka utaratibu mzuri ambao umewawezesha kushiriki kikamilifu Sensa ya Watu na Makazi 2022.
Baadhi ya walemavu hao wamesema walikuwa wanashindwa kushiriki kwenye mambo muhimu ya nchi ikiwemo sensa, kutokana na imani potofu zilizosababisha wengi wao kufichwa.
“Utaratibu uliowekwa na serikali ya Rais Samia kuhusu walemavu kushiriki sensa uko vizuri, hauna changamoto tunamshukuru sana,” amesema Said Hamisi.
Naye Hamis Ally, amesema kuwa amehamasika kushiriki sensa kutokana na utaratibu mzuri na hamasa ya Rais Samia Suluhu kuwataka watu wote washiriki, wakiwemo wenye ulemavu, ili kuweka mipango mizuri ya maendeleo ya wananchi wake.
Mratibu wa Sensa Mkoa wa Mtwara, Tamali William amesema serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), walishirikisha kundi la walemavu kuanzia mwanzo wa uhamasishaji, ambao pia walishiriki katika mafunzo ngazi ya mkoa na wilaya.