Hamisi Shaban Taletale maarufu kama Babu Tale ambaye ni mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM) pia ni meneja wa Msanii Diamond Platnumz ameandika kwenye ukurasa wake wake Instagram matamanio ya kuona kundi la muziki lililowahi kufanya vizuri miaka ya nyuma, Yamoto Band likaandaa tamasha la kumshukuru Mkubwa Fella kwa jinsi alivyowapigania katika safari ya vijana hao kwenye muziki.
“Kwa hakika natamani kuona kundi hili lilowahi kuundwa na mbosso, Enock Bella, Beka Flavor na Aslay wanaandaa Tamasha la kutambua, kushukuru na kumpongeza MKUBWA FELA, ndio wakiandaa onyesho hili itakuwa wameenzi mchango wake kwa vitendo, na nayaongea haya kwa pumzi hii niliyojaaliwa leo,” aliandika Tale.
Pia aliandika ya kwamba anatamani Mkubwa Fella akajengewa sanamu lake pale Temeke kwa kusema kwamba kazi ya kukuza msanii inahitaji miaka mingi lakini yeye aliweza kukuza vipaji vya wasanii wanne kwa muda mfupi.
Kundi hilo la Yamoto Band lilianzishwa mwaka 2014 na baadaye kutamba na ngoma kali kama ‘Najuta’, ‘Niseme’, ‘Nitakupwelepweta’, ‘Cheza kwa Madoido’ na nyingine kibao na miaka mitatu baadaye yaani mwaka 2017, historia ikafika mwisho na kuvunjwa.