Katika maisha ya kila siku, pale mtu anapokuwa kwenye changamoto, baadhi ya watu huzitumia kupima uthabiti wa mahusiano waliyonayo na marafiki zao.
Inapotokea marafiki wakashindwa kuwasaidia wakati wanapopitia changamoto hizo, huwaona kama watu wasio na nyongeza katika maisha yao na hivyo hupitisha chujio wakichuja wale wanaofaa na kuwatenganisha na wale wanaowaona hawafai.
Uamuzi huo huenda siyo sahihi mara zote kwani unaweza kukufanya ukawaondoa maishani mwako watu ambao walikuwa na nia ya dhati na wewe.
Usininukuu vibaya! Ni kweli rafiki zetu wanapaswa kuwa msaada wetu katika shida lakini kabla haujaamua kumfuta mtu katika kurasa za maisha yako, huenda yapo maswali ambayo unapaswa kujiuliza. Ni yapi hayo, endelea kuperuzi hapa.
Nafasi na uwezo wa kukusaidia
Huenda kwa kutazama, unaweza kusema rafiki yako yuko vyema kiuchumi lakini siyo busara kuwaza hivyo kama haujui mwenendo wa hali yake kiuchumi.
Maisha yanavyotupeleka kasi, kuna muda tunasahau kuwa changamoto tulizo nazo siyo zetu tu.
Kabla haujamchuja rafiki yako, walau waza kama kweli mambo yamemnyookea kama unavyodhani.
Wewe ni mtoaji au mpokeaji?
Huenda tunakuwa wepesi kuhamishia lawama kwa rafiki zetu pale wanaposhindwa kuwa wa msaada bila kuwaza kama sisi wenyewe tuliweza kuvaa viatu vyao kipindi walipokuwa kwenye changamoto zao.
Urafiki ni pande mbili na siyo wa upande mmoja. Mnatakiwa kuwa wote mnasaidiana, na siyo wewe kusaidiwa kila siku. Siyo kifedha tu, kimawazo, kihisia na mambo mengine yafaayo rafiki kusaidia.
Unaposema hauhitaji “fake friends” yaani marafiki feki, jihakikishie kuwa wewe nawe ni rafiki mzuri. Huwa unasaidia rafiki zako wanapokuwa na uhitaji na pia huwa unaonekana pale wanapokuhitaji walau kihisia.
Hakikisha huwa unashiriki furaha na huzuni zao na siyo tu wewe kuwa mpokeaji wa msaada wao wakati wewe sio mtoaji pale wanapokuwa kwenye shida.
Nie leo tu ama siku zote?
Huenda rafiki yako amekuwa wa msaada kwa muda mrefu lakini “hapana” yake ya leo ndiyo inakufanya uwaze uthabiti wake kama rafiki.
Kabla ya chujio kupita, hakikisha unakumbuka wema wa awali ambao rafiki huyo amekufanyia.
Muda mwingine, waza kama uliwahi hata kuulipa walau kwa kumweleza thamani yake katika maisha yako.
Na mara nyingine, msaada siyo fedha tu. waza mambo mengine ambayo rafiki huyo amehangia katika maisha yako. Inaweza kuwa connection, stara na hata uwepo kihisia.
Tuvuti ya Bustle inaenda mbali kwa kusema, vigezo vya marafiki wazuri ni pamoja na uaminifu, sapoti, wanokukubali kama ulivyo na wanaokusikiliza na kujaribu kutafuta suluhu ya changamoto zako.
Fahamu kuwa, “hapana” moja, haitoshi kukufanya uingie kwenye orodha ya watu waliopo kwenye simu yako na kufuta ukiona hawawezi kukufaa abadani.
Kazi ni kwako wakati ukiandaa chujio lako.
SOURCE: NUKTA HABARI