Fahamu mambo atakayofanya Rais Samia Uturuki

HomeKitaifa

Fahamu mambo atakayofanya Rais Samia Uturuki

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Uturuki kuanzia leo Aprili 17 hadi 20, 2024 kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan ikiwa na malengo mbalimbali ikiwemo kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba aliyekuwa akizungumza na wanahabari Aprili 15, 2024 jijini Dar es salaam amesema kutokana na uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu baina ya mataifa haya mawili, ziara hiyo itakuwa sehemu ya kushamirisha mahusiano hayo.

“Lengo la pili la ziara hii ni kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya nchi yetu na Uturuki, nchi yeti inahitaji mtaji na teknolojia ambayo Uturuki wanayo, nchi yetu inahitaji masoko ya bidhaa zetu, nchi yetu inahitaji wawekezaji kutoka Uturuki waje hapa,” amesema Makamba.

Makamba ameongeza kuwa kutokana na nchi hiyo kuwa miongoni mwa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani (G20) ni muhimu Tanzania kuendelea kutunza mahusiano na taifa hilo kwa kuwa tutanufaika.

Kwa mujibu wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Kampuni za Uturuki zimewekeza nchini mtaji wenye thamani ya Dola milioni 414.23 za Marekani sawa na Sh 1.1 trilioni za Tanzania.

Makamba ameongeza kuwa lengo la tatu ni ushirikiano kwenye maendeleo, kutokana na taifa hilo kushiriki juhudi za maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwamo huduma za kijamii kama maji, elimu, na afya.

Mambo atayofanya Rais Samia Uturuki

Kwa mujibu wa Makamba, Rais Samia atafanya mazungumzo rasmi ya kiserikali baina yao na kisha kuzungumza na vyombo vya habari ambapo mazungumzo hayo yatahusu maeneo ambayo Tanzania inashirikiana na Uturuki na kuangazia fursa mpya za ushirikiano.

“Baadae kutakuwa na kubadilishana zawadi, kama ilivyo ada katika ziara hizi na baadae kutakuwa na dhifa ya kitaifa ambayo imeandaliwa na mwenyeji wake Rais wa Uturuki,na baada ya hapo itakuwa shughuli za kiserikali zimekwisha,” amebainisha Makamba.

Sambamba na hayo Rais Samia anatarajiwa kwenda Instanbul kushiriki kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uturuki ambapo Rais Samia atazungumza na wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa wa taifa hilo linalopatikana kwa kiasi kikubwa Asia Magharibi.

Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais Samia nchini humo ambao anaenda ikiwa imeoita miaka 14 tangu Rais wa Tanzania alipotembelea taifa hilo lililoasisi mahusiano ya kidiplomasia na Tanzania tangu miaka ya 1963.

Uturuki walifungua ubalozi wao wa kwanza Tanzania mwaka 1979 na kuufunga mwaka 1984 kufuatia changamoto mbalimbali lakini ulifunguliwa tena mwaka 2009 na Tanzania imefungua ubalozi nchini Uturuki mwaka 2017.

error: Content is protected !!