Pato la Taifa lapaa kwa 5.1%

HomeKitaifa

Pato la Taifa lapaa kwa 5.1%

Taarifa ya hali ya uchumi wa taifa imeonyesha ongezeko katika Pato Halisi la Taifa kwa kufika ashilingi bilioni 148,399.76 kutoka shilingi bilioni 141,247.19 mwaka 2022.

Ukuaji huo wa asilimia 5.1 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 unaifanya Tanzania kuendelea kuwa kitovu cha uwekezaji na nchi yenye uchumi unaokuwa kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Sababu zilizochangia ukuaji wa Pato la Taifa ni pamoja na mikakati bora ya kukabiliana na athari za vita ya Ukraine na Urusi, uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji, kuongezeka kwa uzalishaji wa madini na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi.

Uchumi wa Tanzania umeanza kuimarika tena na kwa viwango vya juu baada ya kuathiriwa na athari za Uviko-19 mwaka 2020 na mwanzoni mwa mwaka 2021.

Sekta zilizokuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji mwaka 2023 ni pamoja na sanaa na burudani iliyokuwa kwa asilimia 17.7, fedha na bima asilimia 12.2, madini asilimia 11.3, malazi na huduma za chakula asilimia 8.3 na habari na mawasiliano asilimia 7.6.

error: Content is protected !!