Rais wa Guinea kufanya ziara ya siku tatu Tanzania

HomeKimataifa

Rais wa Guinea kufanya ziara ya siku tatu Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau na Mwenyekiti wa Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika Kudhibiti Malaria (ALMA), Mheshimiwa Umaro Sissoco Embaló, atafanya ziara rasmi ya siku tatu nchini Tanzania kuanzia tarehe 21 hadi 23 Juni 2024.

Lengo la ziara hii ni kuimarisha na kuboresha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Guinea Bissau pamoja na kufungua fursa za ushirikiano katika sekta muhimu kama uzalishaji wa zao la korosho, juhudi za kudhibiti Malaria kupitia Taasisi ya ALMA, na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Vilevile, ziara hii inalenga kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili, hasa kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), ambalo Tanzania na Guinea Bissau ni wanachama.

Ziara hii inatarajiwa kutoa nafasi kwa Tanzania na Guinea Bissau kujadili kwa undani mikakati ya kupambana na kudhibiti Malaria, kwa kuzingatia kuwa Mheshimiwa Rais Umaro Sissoco Embaló ni Mwenyekiti wa ALMA, taasisi iliyoundwa mwaka 2009 na Viongozi wa Nchi zote 55 za Afrika kwa lengo la kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030.

Ikumbukwe kuwa, wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwaka 2023, Mwenyekiti wa ALMA, Mheshimiwa Rais Umaro Sissoco Embaló, alizitambua nchi saba ikiwemo Tanzania kwa kuanzisha matumizi bora ya Kadi ya Alama ya ALMA (ALMA Scorecard) ambayo inahimiza uwajibikaji na hatua mbalimbali dhidi ya Malaria.

Kupitia mpango huu, Tanzania ilitoa mafunzo kwa Wabunge, Viongozi wa ngazi mbalimbali, na watoa huduma za Afya juu ya jinsi ya kutumia kadi hiyo ya alama ili kuhamasisha uwajibikaji na kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya Malaria.

error: Content is protected !!