Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Kamati ya Wakazi wa Magomeni Kota, wameanza kukabidhi nyumba kwa watu 100 kati ya 644 wanaopaswa kukaa kwenye nyumba hizo huku kipaumbele kikiwa kwa wazee na wenye mahitaji maalumu.
Ofisa Miliki wa TBA, Emmanuel Pesambili alisema kazi ya kuwakabidhi nyumba hizo wahusika 644 wote inatarajia kukamilika kwa siku 10 kuanzia jana na kisha wamiliki wake watapewa siku maalumu za kuhamia hapo.
“Wazee na wenye mahitaji maalumu tutawapa kipaumbele cha kwanza na watapewa nyumba za chini. Tutaanza kukabidhi nyumba kwenye jengo la Block 1. Kazi ya kuwakabidhi nyumba ikikamilika tutawapa taarifa ya kuhamia rasmi. Suala la gharama za kununua nyumba hizo bado linafanyiwa kazi,” alisema Pesambili.
Baadhi ya wakazi hao akiwemo Steven Lyao(80) alisema amefurahi kukabidhiwa nyumba yake ya vyumba viwili vya kulala, sebule, badu, choo, jiko na sehemu ya kufulia nguo iliyopo ghorofa ya kwanza.
“Sijawahi kulala kwenye ghorofa, hii ni mara yangu ya kwanza , nimefurahi sana,” alisema Lyao.