Njia sahihi za kukuza biashara yako kupitia mtandao (Digital Marketing)

HomeBiashara

Njia sahihi za kukuza biashara yako kupitia mtandao (Digital Marketing)

Biashara na matangazo ya karne ya 21 yanategemea sana teknolojia. Tunaishi ulimwengu wa dijitali hivyo kila kitu hakina budi kufanywa kidijitali.

Unaweza kuwa na biashara yako au kampuni yako inayotoa huduma au bidhaa imara ya uhakika kabisa lakini usipotumia bidii kujitangaza ama kujiweka mtandaoni, unaweza kuzidiwa na watu ambao huduma zao hazina ubora zaidi yako.

Kujitangaza (kutafuta masoko) kimtandao ni njia rahisi na isiyo gharama kubwa ya kuwafikia watu wengi zaidi. Ukweli ni kwamba usipofanya matangazo ya biashara yako, yote uyafanyao yataishia kwa watu wachache tu wanaokuzunguka.

Nenda na wakati
Siku hizi mtu akitaka msaada wa jambo fulani wazo la kwanza kumjia ni kushika simu yake na kuperuzi kuhusu akitakacho. Hapo ndipo hukutana na majibu ya suala alitakalo mtandaoni.

Fikiria wewe hauko mtandaoni, mtumiaji huyu wa intaneti atakufahamu vipi? Atafahamu vipi una duka la nguo Kariakoo? Badilika nenda na wakati, hamia ulimwengu wa dijitali. Wazungu wanaita ‘Digital Marketing’ mbinu ya kutafuta masoko na kujitangaza kupitia majukwaa ya kimtandao kama vile tovuti, mitandao ya kijamii, email, whatsapp na kadhalika.

Unaanzia wapi?
Ni rahisi ingawa waweza kutumia pesa inapohitajika, kujitangaza mitandaoni ni bure kabisa. Ni kama vile ulivyo na akaunti Facebook bila malipo yoyote. Cha msingi ni wewe kujifunza mbinu za uendeshaji na kuchagua njia ipi inakufaa zaidi.

Miliki tovuti yako
Tovuti hasa kwa mashirika, kampuni na biashara kubwa ni kitu cha msingi. Hii huongeza hadhi ya kampuni kwa ujumla, tofauti kubwa kati ya tovuti (website) na mitandao mingine ya kijamii ni namna ya kuweka maudhui. Kupitia tovuti, mtu anaweza kupata taarifa kwa kina kuhusu kampuni au bidhaa. Pia kwenye tovuti kunaweza kufanyika shughuli kama manunuzi ya mtandaoni, kuandikisha watu kwa ajili ya program mbalimbali kama vile ofa na bidhaa mpya zinazopatikana.

Mitandao ya kijamii
Tanzania kwa sasa kuna watumiaji wa intaneti takribani milioni 23. Maana yake ni kwamba soko lipo huko kwa sababu ndiko watu waliko. Cha kufanya ni kupeleka biashara yako huko. Fungua akaunti kwa jina la biashara au kampuni yako na uanze kujitangaza.

Nini cha kupost ukiwa huko?
Hapa ndipo wengi hukosea, Baadhi ya kampuni hapa nchini hazifahamu namna ya kutumia mitandao ya kijamii.
Mitandao ya kijamii ni watu, hivyo kama kampuni au biashara inatakiwa ifahamu namna ya kuishi na kushirikiana na watu. Isiwe kila siku mnaweka bidhaa zenu tu, utawachosha watu.

Unaweza ukawa unapost picha za bidhaa zako, picha za wateja wenye nyuso za kuridhika na huduma yako. Kama utakuwa mtundu zaidi waweza tengeneza vipande vifupi vya video. Jambo la msingi kuzingatia ni kwamba mitandao ya kijamii ni majukwaa tofauti tofauti yenye maudhui na makundi ya watu tofauti. Ni muhimu kufahamu hili ili uweze kutambua kipi cha kufanya ukiwa kwenye haya majukwaa.

WhatsApp ni fursa
Kwa kaiwaida WhatsApp hujumuishwa kwenye kundi la mitandao ya kijamii. Lakini kiuchambuzi zaidi, WhatsApp pamoja na majukwaa mengine kama Telegram na Messenger yanaitwa private messaging platforms. WhatsApp imekuwa kimbilio la wajasiriamali wengi wa Kitanzania. Kupitia makundi na status watu wanatangaza bidhaa zao na kupata wanunuzi.

Weka biashara yako katika mtandao wa Google My Business
Kampuni ya Google ina mfumo wa kukuwezesha kuweka biashara yako kwenye ramani ya Google ili watu wa karibu na eneo lako waweze kukuona wakitafuta huduma au bidhaa inayoendana na yako. Pia wanaweza kuacha maoni kama vile kukupa nyota tano (fivestar rate) ili kuongeza kuonekana kwa biashara yako mtandaoni.

Pia kuna tovuti nyingine zinazokuwezesha kuorodhozesha biashara au bidhaa yako kama vile Kupatana na Zoom Tanzania.

Kuwa mbunifu katika maudhui (Content Marketing)
Kila mtu anaandika maudhui mtandaoni iwe ni mstari mmoja kama status za Facebook na WhatsApp lakini yote ni maudhui. Kinachokuja kutofautisha kati ya maudhui mengi yanayoandikwa kila siku mtandaoni ni aina na stadi za uandaaji maudhui hayo.
Mfano mchekeshaji maarufu nchini, Idris Sultan kuna wakati huandika posts kwenye ukurasa wake wa Instagram akitangaza kampuni kama Uber. Uandishi wake ni mwepesi na wenye ucheshi lakini hapo ameweza kutangaza biashara.
Kwa kampuni na taasisi mbalimbali unaweza kuajiri muandaa maudhui na msimamizi wa akaunti za kijamii za kampuni. Hili ni jambo muhimu sana katika ulimwengu wa mawasiliano ya kidijitali.

Chukua hatua sasa!
Siku hizi mambo yanaenda kidijitali, hivyo hata biashara yako haina budi kwenda na wakati. Kama uliwahi kujaribu tovuti au mitandao ya kijamii na haukupata matokeo mazuri basi kuna mahali haukufanya kwa usahihi. Tafuta wataalamu wakusaidie usipitwe na wateja kwa kushindwa kuwa online.

Chukua hatua tekeleza!

error: Content is protected !!