Baada ya kiwanda cha kutengeneza magodoro cha kampuni ya GSM kilichoko Mikocheni mkoani Dar es Salaam kuungua na moto Machi 14, Mmoja kati ya wasimamizi wa kiwanda hicho Salah Mohamed, alisema bado hawajafanya tathmini kujua ni hasara kiasi gani imepatikana ila ni hasara kubwa ambayo wamepata kutokana na sehemu kubwa ya kiwanda kuungua.
“Nilipigiwa simu majira ya saa 12 asubuhi na kaka yangu akiniambia kuwa ‘bwana GSM foam Mwenge pale panawaka moto, hebu anagalia nini tunaweza kufanya’. Kwahiyo nikafika haraka na kuanza kufanya mawasiliano. Ninalishukuru Jeshi la Polisi walifika mapema tu.” alisema Salah.
Ezack Abdulrahaman ambaye ni mfanyakazi katika kiwanda hiko anasema moto ulianza kuwaka majira ya 11:30 alfajiri ambapo walipewa taarifa na mlinzi wa kiwanda hiko. kiwanda hiko kina sehemu tatu, lakini eneo lililoathirika na moto huo ni linalotumika kuzalisha magodoro hivyo magodoro pamoja na mashine zinazotumika kuzalisha zimeungua na moto.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema moto ulioteketeza kiwanda hicho ulidhibitiwa usilete madhara nje ya eneo hilo, Sambamba na hayo Kamanda Muliro alimpongeza Kamanda wa zimamoto pamoja na vikosi vingine vilivyoshiriki katika kukabiliana na moto huo.