Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema mwezi uliopita imekusanya Sh trilioni 2.06 katika lengo la kukusanya Sh trilioni 1.98 taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Alphayo Kidata jana ilieleza kuwa makusanyo ni sawa na ufanisi wa asilimia 103.6 na ukuaji wa asilimia 23.17 ikilinganishwa na Machi mwaka jana ambapo makusanyo yalikuwa Sh trilioni.
“Ifahamike kuwa, makusanyo haya kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na kuongezeka kwa uhiari wa kulipa kodi, kuimarika kwa mahusiano baina ya TRA na walipa kodi kunakochagizwa na utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipa kodi kwa wakati,” alisemma Kidata.
Kidata alisema TRA inatoa shukurani na pongezi kwa walipakodi na wadau kwa kujitoa kwa dhati katika kuendelea kulipa kodi kwa wakati.
“Kipekee, tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa miongozo na msaada wake katika kutekeleza wajibu wetu,” alieleza.
Aidha, Kidata alibainisha kuwa ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, pamoja na mambo mengine TRA imepanga kuanza kutumia rasmi mfumo ulioboreshwa wa kieletroniki wa uwasilishaji wa ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuanzia mwezi huu kwa walipa kodi wote waliosajiliwa kwenye VAT.