Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasihi wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa muhimu kutopandisha bei za vitu kiholela bila utaratibu na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya watakaobainika wanafanya hivyo.
“Nawasihi wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa muhimu kuuza bidhaa husika kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji, watakaobainika kupandisha bei bidhaa muhimu bila utaratibu hatua kali zitachukuliwa dhidi yao” alisema Waziri Mkuu.
Akitoa hutuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2022/2023 Bungeni Dodoma, Waziri Majaliwa amesema serikali inatafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa na kuweka mifumo ya kusimamia masoko ya awali na minada na kuwasihi wazalishaji na wasambazaji kushusha bei za bidhaa walizopandisha.
“Hatua nyingine ni Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa na kuweka mifumo ya kusimamia masoko ya awali na minada, Serikali inawaelekeza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa soko ikiwa ni pamoja na kutotumia kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma kupandisha bei,” alisema Waziri Mkuu.