Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametangaza tarehe 23 Agosti kama siku rasmi ya kuanza Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 na kuzindua nembo leo akiwa Zanzibar leo tarehe 8 mwezi Aprili mwaka 2022 na kutaja matumizi ya nembo hiyo.
Rais Samia alitoa wito kwa watu wote kuweza kutumia nembo hiyo kuanzia siku ya kwanza ya sensa mpaka ya mwisho na katika shughuli zote zinazohusu sensa.
“Shughuli zote za kiserikali na za sekta binafsi watumie nembo hii ili kuitangaza sensa yetu. Kwa mfano wizara,idara, taasisi na wakala wa serikali tumieni nembo hii kuitangaza sensa kwa kuiweka katika machapisho, tovuti zenu na mitandao ya kijamii. Na kwa taasisi ambazo zitakuwa na vipindi vya kuelezea shughuli zao katika televisheni zetu nembo ya sensa itumike wakati wa urushaji wa vipindi hivyo,”
“Aidha, kwa sekta binafsi nembo inaweza kuwekwa kwenye vifungashio za bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa nchini, kama vile maji ukiona kuna kijinembo cha sensa pale na kila mtu anakunywa maji itapendeza sana lakini pia mnaweza kuweka kwenye tiketi risiti ,” amesema Rais Samia Suluhu.
Rais Samia amewasihi watu kushiriki kikamilifu katika zoezi hili la sensa na kuwataka makarani kufanya kazi yao kwa weledi kama ambavyo walivyoelekezwa.