Baba mmoja raia wa Kenya anayeishi Kakamega, ameezua mabati ya nyumba yake na kuyauza ili kupata pesa ya kulipia bili ya mwanae ya hospitali.
Willy Odhiambo amesema kijana wake huyo anasumbuliwa na ugonjwa wa ukosefu wa damu mwilini (anaemia) na amekuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ndogo kaunti ya Butere ambako iligharimu Ksh 10,000 ~ 200258.51 ambayo yeye hakuwa nayo.
Juhudi za kutafuta pesa huku na huko kutoka kwa rafiki zake ziligonga mwamba na kumfanya Odhiambo afikirie kuuza mabati ya nyumba yake marefu kwa Ksh 800 ~ 16020.68 na Ksh 700 ~ 14018.10.
“Mwanangu alikuwa mgonjwa nikampeleka hospitalini. Tuliarifiwa bili ilikuwa imefika KSh 10,000. Nilishindwa nitafanya nini nisijue nitatoa wapi kiwango kama hicho cha pesa,” alisema Odhiambo.
Anaongeza kuwa baada ya kung’oa mabati hayo alifunika nyumba hiyo kwa mifuko ya plastiki.
“Usiku mimi huwa sina imani kwa sababu nikifungua macho ni kama nimelala nje na mtu anweza akatuvamia wakati wowote,” Odhiambo alisema.