Fahamu changamoto alizopitia Rais Samia

HomeKimataifa

Fahamu changamoto alizopitia Rais Samia

Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) uliofanyika nchini Ghana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameeleza changamoto alizopitia wakati akichukua kijiti cha kuongoza nchi.

“Changamoto ya kwanza niliyoipata baada ya kuwa Rais wa Kwanza Mwanamke Afrika Mashariki na kwa Tanzania ni kuaminika, kuwafanya watu wa Tanzania kuniamini kwamba naweza kuongoza nchi kama wanaume wanavyofanya,

“Hiyo ilikuwa changamoto yangu kubwa na nilipaswa kuwaaminisha kwamba naweza kufanya na wanawake wanaweza kufanya hivyo, mwanamke hawezi kufeli na nadhani kwa muda wa mwaka mmoja nimeonyesha nguvu ya mwanamke,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alieleza namna fedha za IMF zilizivyotumika tofauti na nchi nyingine ambao zilinunua vifaa vya kujikinga na Uviko-19 na pia kuelezea mahusiano baina ya Tanzania na Benki ya AfDB.

“IMF walitupatia fedha kwaajili ya kujikwamua na janga la Corona, nchi nyingi walizitumia hizo fedha kununua vitu vya kujikinga na Corona lakini mimi nilijenga shule kuwatenganisha wanafunzi kutoka darasa moja kuwa na wanafunzi 100/120 na sasa ni 45/50,

“Tanzania ina mahusiano mazuri na nchi jirani, Mikoa na Wilaya zetu zimeunganishwa na barabara nzuri. AfDB wametusaidia katika ujenzi wa miundombinu mingi, kwa msaada wa AfDB na Taasisi nyingine za Kimataifa nimefanya vizurI,” alieleza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amezungumzia namna alivyoweza kukuza uchumi mara baada ya kushuka kutokana na janga la Uviko-19.

“Uchumi wetu ulishuka kutoka 6.8% hadi 4% kwa hiyo nilikuwa na kazi ngumu ya kuimarisha uchumi na sasa tunavyoongea tumeweza kupanda hadi 5.2% mwaka 2022 na mategemeo yangu ni kurudi kwenye 6.8% kwa mwaka 2025,” alifafanua Rais Samia.

Rais Samia yupo nchini Ghana kwa ziara ya kikazi kwa siku tatu na pia anatarajia kupokea Tuzo ya mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye Kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ambayo hutolewa kwa Mkuu wa Nchi iliyofanya vizuri zaidi.

Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka katika Mkutano wa AfDB, ambao kwa mwaka 2022 unafanyika Accra, Ghana.

 

error: Content is protected !!