Baada ya miaka nane kupita, Tanzania imepata tena bahati ya kuwa mwenyeji wa ziara ya kombe la dunia barani Afrika ikiwa miongoni mwa nchi tisa ambazo kombe hilo litapita.
Kombe hilo ambalo limeingia Tanzania jana Mei 31, 2022 limeambatana na fursa mbalimbali kibiashara na utalii.
Mara baada ya kuwasili nchini, kombe hilo lilipelekwa ikulu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan pekee ndiye alilishika kama sheria zinavyotaka kisha akatoa hotuba fupi ambapo ameelezea namna Tanzania itakavyonufaika na ujio wa kombe hilo nchini ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii na kuamsha chachu ya kufanya vizuri zaidi katika michezo.
“Mchango wake kiuchumi na kijamii una umuhimu wa kipekee kwa fursa zinazoweza kupatikana lakini kubwa kuitangaza nchi yetu… kwa hiyo ningependa kombe hili pia litoe hamasa kwetu tuweze kuitumia nafasi hii kwa manufaa ya Taifa letu,” amesema Rais.
Hii ni mara ya nne kwa Kombe la Dunia kufika nchini Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza lilifika nchini mwaka 2006 na kupokelewa na hayati Benjamin Mkapa na mara ya mwisho liliwasili nchini mwaka 2013 na kupokelewa Jijini Mwanza na Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.
Sifa ya kombe hilo
Kombe hili limeundwa kwa dhahabu yenye uzito wa kilo 6 iliyotengenezwa kama muundo wa watu wawili wanaoshikilia ulimwengu juu yao. Muundo wa sasa wa kombe Halisi ni wa mwaka 1974 na ni moja ya alama za michezo zinazotambulika zaidi duniani.
Fainali za kombe la dunia hufanyika kila baada ya miaka minne na mwaka huu zitafanyika nchini Quatar ambapo mataifa 54 kugombania kikombe hicho kikubwa kabisa duniani ambapo Afrika itawakilishwa na Senegal,Tunisia, Morocco, Ivory Coast na Cameroon.