Wachochezi bei ya umeme na Loliondo wasakwa

HomeKitaifa

Wachochezi bei ya umeme na Loliondo wasakwa

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema serikali imesema itawashitaki waliohamasisha wananchi wafanye vurugu Loliondo na wanaopotosha kuhusu hali ilivyo kwenye eneo hilo wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na waaandishi wa habari, Msigwa alisema hakuna kikosi cha askari waliotumwa kwenda kushambulia wananchi Loliondo, hakuna utaratibu wa kuwahamisha wananchi wa Loliondo na taharuki inayotengenezwa kwenye mitandao kuhusu hali ya huko haina uhalisia.

“Niwahakikishie wote wanaofanya hivi watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, wanaofanya uzushi watatafutwa na wakipatikana hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria zetu, baadhi ya picha ni za zamani na zimetolewa maeneo ya mbali, tunaendelea kuyafatilia haya yoye kwa umakini,” alisema Msigwa.

Kuhusu bei ya umeme, Msigwa alisema hazijaongezeka na kuongeza kuwa serikali inawatafuta waliozusha suala hilo ili wachukuliwe hatua kwani wamevunja sheria.

“Bei ya umeme ni Sh 356.4 kwa uniti moja kwa kundi la matumizi ya jumla likijumuisha wateja wa majumbani, biashara za kati, taa za barabarani, wateja wenye matumizi madogo wanalipa Sh 122 kwa uniti moja wakitumia chini ya uniti 75 ikijumuishwa na Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT),” alisema Msigwa.

error: Content is protected !!