Rais Samia Suluhu Hassan, ameitaka jamii kupiga vita ubakaji pamoja na mila potofu zinazohalalisha ndoa za utotoni,.
Pia amewataka watumishi wa afya kuacha dharau na uzembe, ili kuwaepusha wasichana na wanawake dhidi ya ugonjwa wa fistula kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Ametoa wito huo leo Julai 5, 2022, wakati wa hafla ya kufungua jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam.
Amesema baadhi ya mila na desturi nchini zinabariki mambo ambayo hayawatendei haki watoto kama kuolewa na umri mdogo.
Alisema kuolewa katika umri mdogo husababisha mimba za mapema, ambazo kwa mujibu wa tafiti za kiafya, ndizo chanzo cha kusababisha ugonjwa wa fistula kwa kuwa huharibu maungo ya kike ya watoto wakati wa kujifungua.
Pia Rais amesema miongoni mwa mambo yanayosababisha vifo vya mama na mtoto ni pamoja na dharau na uzembe wa baadhi ya watumishi wa afya, akitolea mfano tukio lililotokea mkoani Kagera la mama mjamzito kujifungulia getini kutokana na kuzuiwa na nesi asiingizwe kituo cha afya.
“Dharau na uzembe wa watoa huduma za afya zinasababisha wanawake kupata matatizo wakati wa kujifungua, hivyo sekta ya afya ifanye mageuzi, ili kuondoa tatizo hilo pamoja na kuacha kabisa mambo ya kimila, ambayo badala ya kusaidia kuondokana na tatizo yanazidi kuchochea,” amesema.
Alitaja njia nyingine ya kukabiliana na vifo vya mama na mtoto kuwa ni kuweka mfumo utakaowezesha kupatikana kwa madaktari bingwa katika wilaya zote nchini, ili kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi na kuwaondolea usumbufu wa kuitafuta mbali.