Katika siku ya kuadhimisha lugha ya kiswahili duniani tarehe 7 Julai, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameweka wazi mikakati ya serikali katika kukieneza kiswahili pamoja na kukikuza.
Licha ya jitihada zinazofanywa na wananchi katika kuikuza lugha ya kiswahili na kuineza, Rais Samia amefafanua mikakati ambayo serikali ya awamu ya sita inaenda kufanya iweze kufika mbali.
“Baadhi ya mikakati yetu ni pamoja na kuziwezesha ofisi zetu za kibalozi zilizoko nje ya Tanzania, kuhamasisha uanzishwaji wa vya kufundishia Kiswahili kwa wageni ambavyo walimu wake watakua ni vijana waliohitimu katika vyuo vyetu vikuu,
“Pia kuwajengea uwezo wa taaluma ya ukalimani, tafsiri, uhariri, ufundishaji wa kiswahili kwa wageni, utangazaji na uandishi wa Kiswahili watanzania ambao wanajihusisha na taaluma hizo kwa kuwapa mafunzo msasa na kuwapatia nyenzo zitakazo wapatia mbinu za kutekeleza kazi hiyo kwa ufanisi,
“Serikali itatekeleza mkakati wa taifa wa kufanya kiswahili kijiuze. Uzinduzi huu wa leo utaongeza nguvu kazi, miundombinu na bajeti kwa mabaraza, taasisi na vyuo vinavyofundisha Kiswahili ili viendelee kuwaandaa wataalamu zaidi watakaotumika duniani kote,”- amesema Rais Samia Suluhu.
Leo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda pamoja na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angeline Motshekga wamesaini Hati ya Makubaliano ya Kufundisha Kiswahili kwa Shule za Awali za nchini Afrika Kusini.
Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanaunga na serikali katika kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.