Tanzania na Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji zimekubaliana kuanza mashauriano ya kuanzisha ushirikiano katika uboreshaji wa huduma za bandari nchini. Makubaliano haya yamefikiwa wakati wa mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni kati ya Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga, na Mkurugenzi Mtendaji wa Bandari ya Antwerp, Bw. Kristof Waterschoot.
Hatua hiyo, ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Mheshimiwa Alexander de Croo, wakati wa ziara aliyoifanya Rais Samia nchini Ubelgiji Februari 2022.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walikubaliana juu ya umuhimu wa kuimarisha ushirikiano zaidi katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na ushirikiano kati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bandari Tanzania na Bandari ya Antwerp.
Bandari ya Antwerp inashika nafasi ya pili kwa ukubwa Barani Ulaya na ni miongoni mwa bandari kubwa zaidi duniani.
Katika mazungumzo baina ya Balozi Nyamanga na Mkurugenzi Mtendaji wa Bandari ya Antwerp, bandari hiyo imeonesha utayari wa kuanza mashauriano na Mamlaka za Usimamizi wa Bandari Tanzania katika kuangalia maeneo ya ushirikiano yatakayolenga kuimarisha na kuongeza ufanisi wa bandari kwenye utoaji wa huduma zake kwa kuanzia na Bandari za Dar es Salaam na Zanzibar.
Katika kutekeleza azma hiyo, Ujumbe wa Bandari ya Antwerp unatarajiwa kuja Tanzania kati ya Septemba na Oktoba 2022, kwa lengo la kujionea hali halisi ya maeneo yanayohitaji ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili ili kuleta ufanisi zaidi.
Moja ya maeneo yanayotarajiwa kujadiliwa wakati wa ziara hiyo ni pamoja na namna ya kuboresha usimamizi na muundo wenye tija kwa watoa huduma mbalimbali wa bandari; uboreshaji wa miundombinu ya bandari na maeneo mengine yanayohusika na usafirishaji wa mizigo; kuongeza uhimilivu na ushindani wa kibiashara na kujengea uwezo watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na Taasisi nyingine zinazohusika moja kwa moja katika utoaji wa huduma za bandari nchini.
Katika eneo la mafunzo, tayari Bandari ya Antwerp imeanza kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania. Kwa sasa, watumishi wanne (4) wa Mamlaka hiyo wanaendelea na mafunzo ya muda mfupi katika Chuo cha Bandari ya Antwerp.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia balozi zake itaendelea kutumia uzoefu na mafanikio ya taasisi mbalimbali kutoka nchi nyingine duniani kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi wa taasisi zake nchini, ikiwemo Mamlaka za Usimamizi wa Bandari.