Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kwamba kiongozi wa kundi la al-Qaida, Ayman al-Zawahiri, ameuawa kwa shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Marekani mjini Kabul, nchini Afghanistan, wakati wa operesheni aliyoisifia kuwa imetenda haki, huku akielezea matumaini yake kwamba itazipa faraja familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.
Katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia leo kutokea Ikulu ya Marekani, Biden alisema kwamba maafisa wa ujasusi wa Marekani waliifuatilia nyumba ya Zawahiri katika mtaa mmoja wa Kabul, ambako alikuwa akijificha na familia yake.
Rais Biden aliidhinisha operesheni hiyo wiki iliyopita na ikatekelezwa juzi Jumapili. Al-Zawahiri na kiongozi mwenzake mashuhuri wa al-Qaida, Osama bin Laden, wanatuhumiwa kupanga mashambulizi ya Septemba 11. Bin Laden aliuawa na jeshi la Marekani tarehe 2 Mei 2011 nchini Pakistan.