Maagizo ya Rais Samia kwa Chamila

HomeKitaifa

Maagizo ya Rais Samia kwa Chamila

Baada ya kutohudumu katika nafasi ya uongozi  kwa zaidi ya mwaka mmoja, hatimaye Albert Chalamila ameapishwa jana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera huku akitakiwa kuwa mtulivu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Rais Samia Suluhu Hassan alimfuta kazi Chalamila aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Juni 11, 2021 na nafasi yake ilichukuliwa na Mhandisi Robert Gabriel.

Hata hivyo, Rais amemrudisha tena Chalamila katika nafasi ya ukuu wa mkoa akimpeleka mkoani Kagera katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa aliyoyafanya Julai 28, 2022 ambapo aliwateua wapya tisa, kuwahamisha vituo vya kazi saba na wengine 10 kubakia kwenye vituo vyao.

Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa walioteuliwa jana Agosti Mosi 2022, Ikulu jijini Dar es salaam amesema licha ya uchapakazi wake Chalamila si mtulivu wa akili hivyo ataendelea kumfatilia kwa jicho la karibu.

“Wewe ni mfanyakazi mzuri lakini mtundu mno sasa nilikuacha nje kipindi hicho nimeamua kukurudisha, naomba ukakue, ukue akili itulie uende ukafanye kazi unisaidie eneo ulilopangiwa wala hii haina maana ndiyo umemaliza ukikaa hapo umekaa nakuangalia kwa ukaribu sana,” amesema Rais.

Chalamila anachukua nafasi ya Meja Jenerali Charles Mbunge ambaye kwa mujibu wa Rais Samia amerudishwa kulitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

error: Content is protected !!