Warudisha mahari baada ya kuteseka kwenye ndoa

HomeKitaifa

Warudisha mahari baada ya kuteseka kwenye ndoa

Mtendaji wa Kijiji cha Mpwayungu Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Selemani Kibakaya ,amesema wazazi wawili waliowaoza binti zao wenye umri wa miaka 14, wamekubali kurejesha fedha na mifugo waliyopokea kama mahari na kurudi na watoto wao nyumbani baada kugundua kuwa watoto wamekuwa wakiteseka kwenye ndoa zao.

Alisema baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Woman Wake Up (Wowap), ambalo linatekeleza mradi wa sauti yangu, Kibakaya alisema wazazi sasa wanabadilika kutokana na elimu inayotolewa.

“Sasa wazazi wana uthubutu wa kufika kwenye ofisi za kijiji baada ya kugundua kuwa walifanya makosa kuwaoza mabinti katika umri mdogo,” alisema.

Alisema kwa sasa wanaofika ofisini wanaongezeka na isingekuwa vyema wakatajwa, kwani inaweza kuwatia woga wengine wenye nia hiyo.

Alisema walifanya utafiti wakagundua mila za kabila la Wagogo binti akivunja ungo anaweza kuolewa na kijana wa kiume anapobalehe anaweza kuoa na wanaoza watoto bila kuangalia umri.

Kibakaya alisema mkazi mmoja wa Nagulo alioa binti mwenye umri wa miaka 14. Binti huyo akaishi miaka mitatu ndani ya ndoa. Ndoa ikamshinda kwani kijana aliyemuoa aliondoka muda mrefu na kwenda Dar es Salaam kutafuta maisha.

Alisema wazazi wa binti walifika ofisi za kijiji na kutaka ufanyike utaratibu wa kurudisha mahari ili waweze kuondoka na binti yao.

“Tulikaa kikao cha pamoja baina ya wazazi na tukapitisha maamuzi mahari irudishwe ambayo ilikuwa ni shilingi 400,000, mbuzi watatu na magunia matatu ya mtama, wazazi wakarudisha mahari na binti yuko kwa wazazi wake,” alisema.

Pia alisema binti mwingine wa kijiji hicho aliolewa akiwa na miaka 14 akaishi na mwanaume ambaye baadaye alienda mkoani Mbeya kutafuta maisha.

“Wazazi walikiri kufanya makosa kumuoza binti yao, wakakubali kurudisha mahari shilingi 150,000, mbuzi mmoja na gunia mbili za mtama na binti yuko mikononi mwa wazazi wake,” alisema.

error: Content is protected !!