Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5 na barabara unganishi ya kilometa 3.8 litaanza kutumika Septemba 30, 2022.
Akizungumza katika ziara yake jana Septemba 18, 2022 Katibu, wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka amesema serikali imeridhishwa na ujenzi wa daraja hilo la Wami ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 89.
“Daraja hili lilianza ujenzi mwaka 2018, hadi Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani ujenzi ulikua umefika asilimia 47, lakini ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia, kasi imeongezeka kwa asilimia 42 na sasa wataalamu wanatuambia ujenzi umefikia asilimia 89,” amesema Shaka na kuongeza
“Pongezi zetu ziwafikie wakandarasi ndani ya kipindi kifupi tuliambiwa daraja hili lingeanza kazi Septemba 20 tukasema haitawezekana lianze kazi kabla ya chama kufika hili jambo ni kubwa, ni utekelezaji wa ilani ya CCM ibara 55 (d) (1)….; “CCM inaridhishwa, na kazi zinazofanywa na serikali” alisema
Alisema daraja hilo limebeba maslahi mapana ya Watanzania kwa kuwa linakwenda kuunganisha Mikoa yote ya Kaskazini na nchi jirani ikiwemo Kenya hivyo fursa ambazo zitatokana na daraja hilo ni nyingi hasa kiuchumi.