Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Inala, Ali Mkonongo kwa tuhuma za kumuua mke wake, Mariam Yusuph kwa kumpiga na kitu kizito kichwani wakati akiwa amelala kisha kuuchukua mwili wake na kuutupa kisimani kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alisema tukio hilo lilitokea Septemba 18 mwaka huu majira ya saa 6:00 usiku katika Kijiji cha Inala Kata ya Ndevelwa Manispaa ya Tabora mkoani hapa.
Alisema mwanaume huyo alifikia kufanya tukio hilo baada ya kutoka kwa mganga wa kienyeji kupigiwa ramli kwamba atamuona mchawi wake kwenye ndoto.
Baada ya mwanaume huyo kulala akamuota mkewe na ndipo alipoamua kufanya mauaji kwa kutekeleza kile alichokiota ndotoni.